Mbeto: Rais Dkt. Mwinyi yuko tayari kuitumikia tena Zanzibar

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Mgombea wake wa Urais Zanzibar Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi yuko imara huku akijiandaa kutwaa ushindi wa kidemokrasia ili kuiongoza tena Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kipindi cha pili.

Vile vile, Chama hicho kimemtaja Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, atabaki kuwa legelege na tepetepe kwakuwa hayo ndio maisha alioyachagua kuishi.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar
Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo akijibu madai ya Jussa aliyedai kuwa, Rais Dkt. Mwinyi yuko tepetepe kwa akihofia kushindwa Uchaguzi.

Mbeto alisema, kwa haiba na ustawi wa mabadiliko ya Maendeleo makubwa yaliochomoza chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi ni ujinga na upuuzi mtu kusema kiongozi huyo atashindwa Uchaguzi.

Alisema, siku zote Wananchi wanahitaji kuona Serikali yao ikiwatumikia kwa kuwaletea maendeleo ikiwemo kuimarika kwa huduma za kijamii na wananchi wakifaidika nazo.

“Jussa ataendelea kuwa legelege na tepetepe kwakuwa ndio maisha ulioyachagua toka akiwa kijana mdogo. Amekubali mwenyewe kuchagua mkondo huo wa maisha hivyo ajikubali kubaki kama ilivyo,” alisema Mbeto.

Akiuzumgumzia uimara wa Mgombea Urais wa CCM, Mbeto alisema Rais Dkt. Mwinyi yuko imara na madhubuti huku akisubiri siku ya kutangazwa na kuwa Rais kwa kipindi cha pili.

“Kwakuwa tumejiandaa kushinda lazima tuibuke na ushindi usio na longolongo. Sera za chama chetu zimejibu changamoto zote zilizokuwa zikiwatatiza wananchi katika sekta za Maendeleo. Tumetimiza ahadi na wajibu wetu. Ni haki yetu kupata ushindi wa kishindo,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu Mwenezi huyo aliongeza kusema, mkataba wa miaka mitano iliyopita kati ya wananchi na CCM, ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi. “Kazi hiyo kimsingi imefanyika kwa weledi na umakini mkubwa na kukamilika,”

“Rais ametekeleza ahadi za kisera na zile za kibinafsi, hivyo hawezi kushindwa na mgombea anayetaka achaguliwe ili akafanye majaribio ya kuongoza nchi. Serikali si chumba cha maabara cha kufanyia majaribio,” alisisitiza Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi, amewahakikishia Wananchi, Wanachama wa CCM, wafuasi na Wakereketwa wake, kujiandaa na kwenda kupiga kura Oktoba 29, 2025 kisha wawe tayari kupokea matokeo ya ushindi.

“Jussa na wenzako jiandaeni kushuhudia kimbunga cha ushindi wa CCM kikiwapeperusha. Hila na njama zenu zimekwama, hivyo jipangeni kutoka machozi bila kilio,” alisema Katibu Mwenezi huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here