TIMU ya wataalamu kutoka Benki ya ABSA Tanzania imefanya ziara maalum katika miradi mikubwa ya makazi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam — ikiwemo Samia Housing Scheme – Kijichi na Kawe 711 Housing Project.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuwajengea uelewa maafisa wa ABSA kuhusu utekelezaji wa miradi ya NHC, kuonyesha fursa za ununuzi wa nyumba, na kuimarisha ushirikiano katika kusaidia Watanzania kumiliki makazi bora kupitia mikopo ya nyumba.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ABSA Tanzania, Obedi Laiser, ambaye hakuficha furaha yake baada ya kujionea kazi kubwa inayofanywa na NHC katika kubadilisha sura ya makazi nchini.
“Tumepata fursa nzuri ya kujifunza na kujionea kazi kubwa inayofanywa na NHC. Nyumba hizi ni za kisasa, zenye ubora wa juu na zitachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya uhaba wa makazi nchini. Tunawapongeza NHC kwa ubunifu na ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa miradi hii,” alisema Laiser.
Aidha, alisisitiza kuwa ubora wa miradi ya NHC unaendana kikamilifu na falsafa ya chapa ya ABSA inayosema “Hadithi yako ina thamani”, akifafanua kuwa nyumba hizo zinaakisi maisha halisi ya Watanzania na ndoto zao za kumiliki makazi bora.
Kwa upande wa NHC, Meneja Miradi, Injinia Grace Musita, aliyeongoza maelezo kwa niaba ya Shirika, alieleza kuwa miradi ya Samia Housing na Kawe 711 ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“NHC imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora, salama na ya kisasa. Miradi hii inajengwa kwa kutumia teknolojia za kisasa, ubora wa hali ya juu na kwa kuzingatia mazingira rafiki,” alisema Injinia Musita.
Naye, Deogratious Batakanwa, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa NHC, aliishukuru Benki ya ABSA kwa ushirikiano wa muda mrefu katika kusaidia ujenzi na mauzo ya nyumba za Shirika.
“Tunathamini ushirikiano wa ABSA kwa kutuwezesha kifedha katika ujenzi wa miradi yetu, na pia kwa kuwasaidia wateja wetu kupata mikopo ya nyumba. Ushirikiano huu ni mfano bora wa taasisi za kifedha na sekta ya makazi