SMZ kujenga hospitali mbili kubwa za rufaa Z’bar

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga hospitali nyengine mbili kubwa za rufaa zitakazotoa huduma bora za matibabu ya kibingwa kwa maradhi ya moyo, saratani, ubongo na uti wa mgongo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2025, Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Limited.

Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mngereza Miraji Mzee, amesaini kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar, huku Mkurugenzi wa Kampuni ya Jiangxi International, Peng Chao, akisaini kwa niaba ya kampuni hiyo.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa tukio hilo ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini, na kwamba Hospitali ya Mnazi Mmoja inaenda kubadilika kuwa hospitali mpya kabisa yenye hadhi ya kisasa.

Aidha, Rais Mwinyi amebainisha kuwa sekta ya afya ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, kwani wananchi wenye afya bora ndio msingi wa ujenzi wa uchumi imara na uimarishaji wa utoaji wa huduma bora na za kisasa.

Amesema kuwa baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali kuanzia ngazi ya msingi, wilaya na mkoa, hatua inayofuata ni kujenga hospitali tano za rufaa, moja katika kila mkoa, zitakazotoa huduma za kisasa zenye viwango vya kimataifa na kuendeshwa kitaalamu.

Rais Dkt. Mwinyi alizitaja hospitali mbili mpya zitakazojengwa kuwa ni; Hospitali ya Matibabu ya Magonjwa ya Saratani, Moyo na Mifupa na Hospitali ya Rufaa na Kufundishia Watendaji wa Sekta ya Afya, itakayojengwa Binguni.

    Ameeleza kuwa kukamilika kwa hospitali hizo kutaiwezesha Zanzibar kuondokana na utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kwani huduma za matibabu ya kibingwa zitapatikana nchini kwa ubora na viwango vinavyokubalika Kimataifa.

    LEAVE A REPLY

    Please enter your comment!
    Please enter your name here