WETE, Kaskazini Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imeamua kutoa Hatimilki za Mashamba ya Karafuu kwa wakulima ili kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na kuwawezesha wakulima kupata tija zaidi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa hatimilki za mashamba ya karafuu iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, Dkt. Mwinyi amesema kwa muda mrefu wakulima waliokuwa wakiyashughulikia mashamba ya Serikali walikosa tija kutokana na mashamba hayo kukodishwa kwa watu wengine wakati wa mavuno, jambo lililowakatisha tamaa na kudhoofisha juhudi za kuyaendeleza mashamba hayo ipasavyo.
Amesema hatua hiyo ya utoaji wa hatimilki itaondoa migogoro ya mipaka ya mashamba baina ya wakulima na kuimarisha umiliki halali wa mashamba yao.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya uzalishaji wa karafuu, ikiwemo kuimarisha mfumo wa ununuzi kupitia Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) ili kuwaondolea wakulima changamoto za uuzaji.
Amesema mfumo huo wa kidijitali umehakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati, kupitia benki au miamala ya fedha kwa njia za mtandao.
Aidha, Dkt. Mwinyi amesema ZSTC imeanza kutumia mfumo wa ZSTC Buying Mobile, ambapo maafisa wa shirika hilo hufika kwa wakulima moja kwa moja na kununua karafuu zao kwa malipo papo kwa hapo, hatua inayoongeza ufanisi na tija kwa wakulima.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa Serikali inaendelea kugawa bure miche ya mikarafuu ili kuhamasisha upandaji mpya, sambamba na kutenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya mikopo na pembejeo kwa wakulima wa karafuu.
Amewataka wakulima waliopatiwa hatimilki kuyatunza mashamba yao na kuyaendeleza kwa bidii ili kilimo hicho kiendelee kuwapa manufaa wao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Vilevile, ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kuhakikisha zoezi la utoaji hati linafanyika kwa mafanikio.