Wazanzibar wanataka maendeleo, sio maneno – Mbeto

0

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ys Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema, Wazanzibar wanataka maendeleo sio maneno ya kwenye Khanga.

Mbeto, alisema wapinzani wao wamekuwa wakizungumza maneno matupu bila kuweka wazi watawafanyia nini Wazanzibar wakipewa dola, lakini Rais Dkt. Mwinyi amefanya mambo yanayoonekana kwa macho.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Kampeni uliofanyika leo, Oktoba 7, 2025 kwenye uwanja wa michezo wa Likoni, Kojani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mwenezi huyo alisema, Rais Mwinyi ni kiongozi wa kuchora ramani ya maendeleo na amedhihirisha hilo kwa mambo makubwa aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema, wananchi wa Kojani walimuomba awajengee kituo cha afya na boti la kubebea wagonjwa, mambo ambayo yote ameyatekeleza, ambapo kituo cha afya kinaendelea kujengwa.

“Ulipokuja Kojani kwenye mambo ya elimu, wananchi waliomba kituo cha afya na boti la kubebea wagonjwa, leo nafurahi ahadi zote mbili umezitimiza. Tunapokupa sifa, hatukupi sifa ambazo sio zako, bali ni kutokana na mambo unayoyafanya,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa, ahadi kama hiyo Dkt. Mwinyi ameitekeleza kwa wananchi wa Tumbatu.

Akifafanua zaidi alisema, kituo hicho kikimalizika, wananchi wa Kojani watapata huduma zote ikiwemo upasuaji mdogo na akinamama wajawazito watajifungua kwenye kituo hicho, na boti litawasaidia kusafirisha wagonjwa iwapo kutatokea tatizo kubwa.

Kutokana na kazi hiyo kubwa aliyoifanya, Mbeto alimshukuru Dkt. Mwinyi na kusititiza kuwa “kazi unayoifanya Wazanzibar wenzio tunaiona na kila mwenye macho anaona.”

Mbeto alisema, maendeleo ambayo yamefanyika kwa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Nane ndio wanayoyataka Wazanzibar, “Wanataka amani ya nchi yao na nafsi zao, lakini wanataka maendeleo ya nchi yao. Moja ya maendeleo ni afya, ukikosa afya hutoweza kufanya kazi.”

Alisema, Rais Dkt. Mwinyi amefanya kazi kubwa katika kuboresha sekta ya afya sambamba na kutengeneza mazingira mazuri ya upatikanaji wa wa elimu kwa watoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here