MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi wa Shumba Mjini kuwa Serikali itaendelea kuimarisha Bandari ya Shumba ili iwe chanzo kikuu cha ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Pemba.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuifanya Bandari ya Shumba kuwa ya kisasa yenye uwezo wa kupokea meli kubwa za mizigo na kuwa kitovu cha shughuli za uvuvi wa kisasa, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumzia suala la fidia kwa wananchi waliotoa maeneo yao kupisha mradi wa bandari hiyo, Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa Serikali itawalipa fidia zote kwa haki na uwazi, na kueleza kuwa jambo hilo linashughulikiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kila mwananchi anapata stahiki yake.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 6, 2025, alipokutana na wanachama wa CCM na wananchi wa Shumba Mjini, Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni kisiwani humo, ambapo ameahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika awamu ijayo.
Aidha, amewaomba wananchi kumuamini tena na kumpa kura ya “Ndiyo” pamoja na wagombea wa CCM katika nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, ili Chama Cha Mapinduzi kipate ushindi wa kishindo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita.
Mapema, Rais Dkt. Mwinyi amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Alasiri katika Msikiti wa Ijumaa wa Shumba Mjini, ambapo amewasihi waendelee kuiombea nchi iendelee kuwa na amani, umoja na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu.