Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimemtaja Mgombea Urais wa Zanzibar Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni zawadi itakayoifikisha Zanzibar katika kilele cha Ustawi wa Jamii, demokrasia na Maendeleo ya Uchumi.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis katika mikutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mbeto alisema, ifikapo Mwaka 2030, Serikali ya Zanzibar chini ya CCM, itakuwa na Uchumi unaojidhatiti ikiwemo kupanda kwa viwango vya utoaji wa huduma bora za jamii.
Mbeto alisema, msukumo uliopo katika utekelezaji wa sera chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi akisaidiwa na watendaji SMZ, sekta ya Umma na binafsi, Uwezeshaji na Ushirikishwaji Wananchi, yatatokea mageuzi ya aina yake.
Alisema, Zanzibar itapanda chati na kuzivutia kampuni za Kimataifa, Wawekezaji wenye nguvu za mitaji duniani, kuja kuwekeza miradi ya kiuchumi Zanzibar, Biashara, elimu na teknolojia.
“Rais Dkt. Mwinyi ni zawadi ya thamani kwa maendeleo ya jamii. Mafanikio ya kisera yatazidi kufungua milango ya fursa za kiuchumi, ajira na kubadili taaswira nzima ya maisha ya jamii,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu Mwenezi huyo alisema Maendeleo yoyote lazima yakuzwe na uwekezaji wa Mitaji mikubwa, Uwazi, Uwajibikaji, Ustawi wa demokrasia na kuwashirikisha Wananchi katika maamuzi.
“Ongezeko la ajira katika dunia ya sasa lazima iambatane na ushawishi wa mpango shirikishi na mikakati ya uwekezaji kiuchumi. Maendeleo hatokea kwa mipango ya muda mfupi na mrefu,” alisisitiza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi aliitaja Zanzibar ya sasa chini ya Rais Dkt. Mwinyi ni kama ndege iliosheheni nyenzo za maendeleo kikiwa katika mistari ya zebra ikisubiri kupaa angani na kutua salama.
“Rais ajae toka CCM kuanzia Mwaka 2030 hadi 2040 ataikuta Zanzibar yenye Miumdombinu bora. Kazi itakayofanyika Mwaka 2025 hadi 2030 itamrahisishia utekelezaji wa kisera na mikakati,” alieleza.
Vile vile, Mbeto alimtaja mgombea huyo wa Urais wa CCM ni kiongozi aliyejaaliwa karama ya uongozi, uthubutu, nia njema huku akitaka kila mwananchi apate huduma na maisha bora.