MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Awamu ijayo imeweka malengo maalum ya kuiletea Zanzibar maendeleo makubwa zaidi.
Akihutubia leo, Septemba 2,2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo wa Bumbwini Kidimni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dkt. Mwinyi amesema kuwa amani, mshikamano na utulivu ni nguzo kuu za maendeleo ya nchi.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi ameeleza mambo kadhaa ambayo Serikali itayatekeleza, ikiwemo:
✅ Elimu: Kuendelea kuboresha skuli za kisasa na kuongeza ufaulu katika ngazi zote za elimu.
✅ Huduma za Maji: Kusambaza maji safi na salama katika maeneo yote ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
✅ Afya: Kuendeleza ujenzi wa hospitali za mikoa ili kuboresha huduma kwa wananchi.
✅ Miundombinu: Kukamilisha ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, mradi utakaofungua fursa za kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
✅ Fidia ya Wananchi: Serikali imetenga shilingi bilioni 11 kwa fidia ya wananchi waliopisha mradi wa bandari.
✅ Uhakika wa Chakula: Ujenzi wa maghala ya chakula ili kudhibiti bei na kuhakikisha usalama wa chakula.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kupuuza propaganda dhidi ya kura ya mapema, akibainisha kuwa ni haki ya kisheria kwa vikosi vya ulinzi na usalama.
Mwisho wa hotuba yake, aliwaomba wananchi kukichagua CCM akisisitiza kuwa ndicho chama pekee kinachotekeleza ahadi zake, na kuwasihi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili CCM ishinde kwa kishindo.