Mbeto: ACT kina sera hatari za ukabila na ubaguzi

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ACT Wazalendo kina ajenda ya siri na Sera za ubaguzi hivyo ni hatari kwa mustakabali wa amani ya Zanzibar na watu wake ikiwa siku moja kitachaguliwa na Wananchi.

Kimeitaja hatua ya Makamu Mwenyekiti wake Ismail Jussa Ladhu, kumshambulia mgombea Urais wa CCM, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi akidai hana asili ya Zanzibar ni ushahidi tosha ACT si chama sahihi.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema ACT kina Sera za kibaguzi na ubaguzi ni hatari kwa ustawi wa Umoja na Mshikamano.

Mbeto alisema, karibu wananchi wote wa Zanzibar, aidha watakuwa na Asili moja ya Zanzibar na nchi nyingine, hivyo ACT kusema kikishinda wasio na Asili ya Zanzibar watarudishwa kwenye Asili zao huo ni ubaguzi mpya.

Akitoa mfano alisema, kwa Zanzibar utawaondoa watu wangapi na kuwaacha wangapi, kwani kulingana na Jiografia ya Visiwa hivyo, ni mkusanyiko wa Asili za watu, makabila na rangi mbalimbali duniani.

“Jussa amekuwa akimnyooshea kidole Rais Dkt. Mwinyi na kudai ana asili ya Mkuranga Tanzania Bara. Cha ajabu Jussa hataji Asili yake ni India. Mtu mwenye Asili ya Mkuranga na India yupi aliyetoka nje ya Bara la Afrika?,” alihoji Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema, katika dunia ya sasa ambayo Mwafrika amezaa na Mjapani, kuna Wachina na Magoa waliozaliwa Zanzibar, na mtu mwenye asili ya Rwanda na Malawi amekuwa Rais wa Kwanza Zanzibar, madai ya Jussa ni zaidi ya upuuzi.

“Zama ya Ubaguzi wa rangi, Asili na ukabila imekwisha duniani. Kiongozi anayebagua wenzake kwa Rangi, Kabila au Asili ni katili kuliko walivyokuwa makaburu wa Afrika Kusini,” alieleza.

Mbeto akimshutumu vikali Jussa, huku akimwita Mwanasiasa mapepe, anayeshindwa kujenga hoja za kisiasa na kuwa mfuasi wa Sera za jikoni zenye mipasho ya unyago na kidumbaki.

“Hutamsikia hata siku moja akinadi sera za chama chake jukwaani. Anachokijua ni mtamko ya ubaguzi, wivu wa wake wenzake na chuki binafsi, ” alisema Katibu huyo Mwenezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here