CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema wananchi wa Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, hawana sababu yoyote ya kutompa kura Dkt. Hussein Mwinyi kutokana na mambo makubwa aliyowafanyia.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema hayo jana, Septemba 28, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Wilayani humo.
Kwenye mkutano huo, Mbeto alitaja mambo kadhaa ambayo yamefanywa na Rais Mwinyi kwa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Nane kwenye wilaya hiyo.
Alisema, Micheweni ya miaka 10 au 20 iliyopita, sio ya hivisasa, ambapo kulikuwa na shida nyingi ambazo Rais Dkt. Mwinyi amezifanyia kazi, ikiwemo ukosefu wa huduma za afya.
Mbeto alisema, kabla ya kujengwa hospitali, wananchi walilazimika kwenda kufuata huduma za afya Wete; “leo hatuendi, tupo hapa Micheweni.”
Mbali na suala hilo, Mwenezi huyo alisema Rais Dkt. Mwinyi ametatua changamoto za wavuvi na wakulima wa Mwani kwa kuwapa boti, sambamba na kujenga bandari maeneo ya Shumba Mjini.
Alisema, bandari hiyo inatarajia kuzinduliwa wakati wowote kuanzia sasa, baada ya kukamilika kwa jengo la utawala, huku bandari nyingine inatarajia kujengwa Wete.
Aidha, Mbeto alisema Rais Dkt. Mwinyi ameboresha miundombinu ya barabara, ambapo amejenga mtandao wa barabara yenye kiwango kizuri ambayo haipo sehemu yoyote ile Unguja na Pemba. “Dkt. Mwinyi ametandika lami kila kona.”
Mbali na hilo, alisema katika shule tatu bora na nzuri za ghorofa ambazo zimejengwa, moja ipo wilayani Micheweni.
Alisema, mara zote amekuwa akirudia suala la malipo wanayopata wazee wanaotimiza umri wa miaka 70, ambapo barani Afrika ni Zanzibar pekee wana mfuko wa pensheni jamii, ambapo kwa Micheweni watu 2,972 wananufaika.
“Ni nchi pekee inayolipa pensheni jamii na Rais Mwinyi amepandisha kiwango kwa asilimia 150,” alisisitiza na kuongeza kuwa, pamoja na mambo yote hayo, Rais Mwinyi anajenga viwanja vya michezo.
Kutokana na hayo machache ambayo aliyataja, Mbeto alisema, wananchi wa Micheweni hawana sababu ya kumnyima kura Dkt. Mwinyi na wagombea wengine wa CCM ili waendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilani mpya ilivyoagiza.