Mbeto: Serikali ya Awamu ya Nane imeboresha maisha ya watu

0

Na Iddy Mkwama

WAZANZIBAR wametakiwa kupuuza maneno yanayotolewa na viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kwamba, Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi haijaboresha maisha ya wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika Kisiwani Pemba, ambapo alisema, katika awamu zote zilizopita, Serikali ya Awamu ya Nane ndio pekee ambayo imeboresha maslahi ya wananchi wake kwa kiwango kikubwa.

Mbeto alisema, kwenye nchi yoyote, Serikali inaangalia maeneo makuu matatu; kwanza kwenye sekta rasmi (sekta ya umma), sekta binafsi na wajasiriamali, ambapo huko kote Rais Mwinyi amezingatia na amefanya maboresho makubwa.

Akianza na sekta rasmi, Mbeto alisema, wakati anaingia madarakani, Rais Dkt. Mwinyi alikuta pensheni kwa wastaafu wenye kipato cha kawaida walikuwa wanapokea Shilingi 90,000, lakini akapandisha kwa asilimia 100, hivisasa mtumishi yeyote anapokea 180,000 na mishahara imepanda kwa ngazi zote.

“Tumekwenda mbali zaidi, mwananchi aliyefikia miaka 70 analipwa, Dkt. Hussein kaikuta pensheni jamii kwa wazee wetu inalipwa 20,000, sasahivi kaipandisha kwa asilimia 150, kwasasa mzee yeyote aliyetimiza miaka 70 analipwa 50,000,” alisema Mbeto.

Alisema, mbali na malipo hayo, wazee wamepewa kipaumbele cha matibabu bure na popote wanapokwenda kufuata huduma kwenye taasisi za umma, “hakuishia hapo, kuna wazee wetu ambao tunawatunza pale Limbani, Sebleni, na Welezo, Rais Mwinyi kwa wazee wanaotunzwa kwenye maeneo haya, wanalipwa 40,000; wanakula bure, wanatibiwa bure na huduma zote bure.”

Alisema, pamoja na huduma zote hizo, Mzee anayelelewa kituoni, anapata Shilingi 50,000 ya pensheni jamii, kwa maana hiyo mzee huyo anapata Shilingi 90,000 kwa mwezi wakati anakula na kulala bure.

“Hakuna nchi yoyote Afrika ambayo inafanya hivi. Haya hawayasemi, ndio maana kwenye mikutano yao unakuta wanalalamika tu; ubaguzi, hausikii wao watafanya nini, niwahakikishie hakuna awamu ambayo imeboresha maisha ya watu kama awamu hii ya Rais Mwinyi.”

Kwa upande wa sekta binafsi, alisema kima cha mwanzo kimewekwa isipungue 350,000 na serikali inasimamia, pia kupitia wizara ya kazi, serikali imekuwa ikisimamia haki za mikataba ya wafanyakazi ili kuhakikisha haki zao zinapatikana.


“Katika suala hilo serikali imekwenda mbali zaidi, michango yote ya watumishi wa serikali na sekta binafsi, lazima iwasilishwe kwenye mifuko ya hifadhi ili wanapostaafu au wanapopata matatizo wapewe mafao yao,” alisema Mbeto.

Mbali na hilo, alisema Rais Mwinyi ndiye aliyeelekeza mifuko kutoa fao la kupoteza ajira, ambapo hivisasa ukipoteza ajira unapewa michango yako yote, pia kuna mafao ya uzazi na dharura. “Yote haya ni mazingira ambayo ameyaweka Dkt. Mwinyi ili kuhakikisha wananchi wake wanafaidika.”

Aidha, kwa upande wa sekta inayohusisha wajasiriamali, serikali ya Awamu ya Nane, imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 55. “Kwanza alichofanya, amejenga masoko kila halmashauri, zaidi ya Bilioni 16 zimetumika kujenga maeneo bora na mazuri ya wananchi kufanya biashara zao.”


Alisema, pamoja na masoko hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza wote waliopewa masoko wapewe mikopo kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) na halmashauri inatoa mikopo ambayo inaitwa 4-4-2 kwa ajili ya vijana, akinamama na walemavu.

“Ukiacha masoko kila halmashauri, katika kuhakikisha wafanyabishara na wajasiriliamali wanapata mikopo na maeneo mazuri ya kufanyiakazi, Rais Mwinyi amejenga masoko makubwa ya kimkakati. Ukienda Kwerekwe utaliona, ukienda Chuini unaliona, tumewatoa wafanyabiashara kwenye maeneo holela, sasahivi wanafanya biashara kwenye maeneo mazuri na wanatozwa kiwango kidogo sana.” alisema Mbeto.

Aliendelea kusema kuwa, Dkt. Mwinyi kwenye ziara zake, amekuwa akisisitiza kwamba, wafanyabiashara hao watozwe kiwango kidogo, “hizi fedha hatujakopa popote, ni fedha za serikali, hatuna haraka ya kuzirejesha, upenzi huo unapata wapi zaidi ya Serikali ya Awamu ya Nane? Yote ni katika kuwasaidia Wazanzibar wafanye biashara, wapate kipato.”

Aidha, Mbeto alisema Rais Mwinyi amenunua boti zaidi ya 1,500 ambazo zina kila kitu; nyavu, ‘fish finder’ na rada, “leo hakuna taarifa za mvuvi kupotea kama ilivyokuwa wakati ule wa uvuvi wa ngarawa; katoa boti kwa wavuvi na wakulima wa mwani, lakini haya wapinzani hawayasemi.”

Mbeto alisema, baada ya mafanikio waliyoyapa wakulina wa mwani na wavuvi ambao takwimu zao za uvuvi zimeongezeka, Serikali imepanga kununua boti kubwa zaidi na tayari mpango huo umekamilika.

Vile vile, alisema Rais Dkt. Mwinyi amejenga maeneo ya kisasa ya uhifadhia samaki yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5000 kwa wakati mmoja, pia amenunua mashine maalumu za kukaushia dagaa kwa masaa kadhaa.

“Kwa hiyo, Rais Mwinyi amefanya jitihada kubwa za kutatua ugumu wa maisha, kafanya vitu vikubwa, tunakwenda kuanzisha hifadhi ya chakula; Serikali itakuwa inaagiza chakula na kuhifadhi, kwa mwaka mzima tutakuwa tuna chakula, na itasaidia kushusha bei, haya hauwezi kuyasikia huko ACT, maana wao ni Muungano, kusema watu kubagua watu,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here