Na Iddy Mkwama
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amekanusha madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa kwamba ujenzi wa barabara zote za Unguja na Pemba, imekabidhiwa kampuni moja ya IRIS.
Jussa alitoa madai hayo kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, ambapo alisema, mbali na kampuni hiyo kupewa jukumu la ujenzi wa barabara hizo, utaratibu wa zabuni haukufuatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Kisiwani Pemba, Mbeto alisema madai hayo hayana ukweli wowote, kwani utaratibu wote umefuatwa, ambapo kampuni husika ziliomba na zikashinda kutokana vigezo vilivyowekwa.
Kuhusu madai ya kampuni moja kupewa kazi ya ujenzi wa barabara zote alisema, zipo kampuni takribani saba ambazo zinaendelea na ujenzi kwenye maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
“Kuna kampuni ya CCECC ya China, wao walipewa Kilomita 277 kati ya hizo 134 zitajengwa kwenye Kisiwa cha Pemba, barabara ya njia nne kutoka Chake – Mkoani Kilomita 43.5 zitajengwa na Kampuni ya PROPAV ya Brazil ambayo imejenga Uwanja wa Ndege wa Pemba,” alisema Mbeto.
Aliendelea kusema, kampuni ya IRIS ambayo imetajwa na Jussa, ina Kilomita 279.95, huku kampuni ya kizalendoya MECCO yenyewe inajenga barabara ya Chake, Wete Kilomita 22 na imefikia pazuri. “Kwa miaka mingi ilikuwa haijakamilika, lakini Serikali ya Awamu ya Nane imeikamilisha.”
Mbeto alisema, kampuni nyingine ni OCLA ZED ambayo nayo ni ya kizalendo, inajenga Kilomita 5.4, barabara ya Mgelama – Wambaa, pia kuna Kilomita 163 imepewa kampuni ya IRIS, kati ya hizo Kilomita 82 zinajengwa Pemba na nyingine ni kampuni ya OLCOM.
“Kwa maana hiyo ni uzushi ambao hauna hata mashiko ambao ndugu zetu wa ACT Wazalendo wanajaribu kuwaaminisha watu,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa, ujenzi wa barabara hizo unaendelea vizuri na barabara zote za Unguja na Pemba zitakamilika.
Akielezea lengo la Serikali inayoongoza na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuanza na ujenzi wa miundombinu ya barabara alisema, ni katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Wachumi wote wanajua, unapoweka miundombinu mizuri, unawarahisishia wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi. Mvuvi anayevua samaki Micheweni au Shumba Mjini, kama hakuna miundombinu mizuri itakayosababisha afike haraka Chakechake na maeneo mengine, yule samaki anaharibika,” alisema.
Aliendelea kusema “Njia moja ya kukuza uchumi ni miundombinu, ndio maana Serikali ya Awamu ya Nane ikasema ije na utaratibu wa ujenzi wa miundombinu kwa kasi. Zamani tulikuwa na mfumo ambao barabara moja mfano kutoka Chake kwenda Wete, inaweza kuchukua miaka mitano, Rais akasema hapana, bora tujenge, kama kuna marejesho, turejeshe.”
Kutokana na mafanikio hayo kwenye upande wa miundombinu, Mbeto aliipongeza Serikali ya Awamu ya Nane ambayo imefikia malengo makubwa zaidi ya vile Ilani ya uchaguzi ilivyoagiza.
“Sisi kwenye ilani iliyomalizika tulielekeza Serikali ijenge Kilomita 196, lakini hadi sasa Kilomita zaidi ya 1000 zinajengwa,” alisema na kuongeza kuwa, barabara hizo zinajengwa kwa kodi za ndani.
“Mfano kwenye tozo za mafuta, kwa kila lita, inakwenda kwenye mfuko wa barabara, lakini ukiacha tozo hii, sote tunamiliki vyombo vya moto, kuna kitu kinaitwa ‘road license,’ kibali cha kutumia barabara,”
“Huko kote kuna kodi mbalimbali ambazo zinatozwa na hizi zote zote zina mfuko maalumu ambazo zinakwenda kuongezea ujenzi wa barabara. Leo hakuna Mzanzibar yeyote asiyeona uadilifu wa Rais Mwinyi katika kuijenga nchi yetu,” alisisitiza Mwenezi Mbeto.