Mbeto: Uongo wa Jussa unakivua nguo chama chake

0

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemkanya Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu na kumtaka aache Siasa za uongo na uzushi kwasababu haziwezi kukipatia hadhi na heshima chama chake.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema hayo katika Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni Jimbo la Fuoni, Mkoa Mjini Magharibi Kisiwani Unguja.

Mbeto alisema, Viongozi wa ACT mara zote wamekuwa wakishindwa kutofautisha kati ya hatari ya uongo katika Siasa na ukweli na uwazi unaoambatana na dhana ya Siasa safi na uongozi bora.

Alisema, madai ya Jussa kuhusu bei ya karafuu, si kwamba yamekivua nguo chama chake, lakini pia yanaendelea kumpunguzia heshima yake mbele ya jamii na kumfedhehesha na kuonekana ni Mwanasiasa kituko.

“Bei ya Karafuu ilipanda katika utawala wa Rais Mstaafu Dkt. Ali Mohamed Shein kutoka Shilingi 3000 hadi kufikia Shilingi 14000 kwa Kilo moja,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, bei ya karafuu ilipanda tena Dkt. Shein akiwa madarakani ili ilingane na soko la dunia na kufikia Shilingi 21000, hadi sasa bei ya karafuu ni Shilingi 13000 kwa kilo.

“Mwambieni kibaraka Ian Smith wa Zanzibar apunguze chumvi ya uongo wake. Uongo na Uzushi unampunguzia uaminifu na heshima kwa Wananchi, amekuwa Mwanasiasa Komedi mwenye vibweka,” alisisitiza.

Mbeto aliitaja Serikali ya Rais Mstaafu Shein ndio iliopandisha bei ya karafuu, hivyo Jussa anapodai bei ilipandishwa na Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, huo ni aina mpya ya uongo akimzulia Marehemu.

Aidha, alisema kabla na baada ya Mapinduzi Mashamba ya Karafuu Kisiwani Pemba, Serikali iliwakodisha Wakulima wa karafuu, jambo ambalo Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi ilipoingia madarakani, mashamba hayo sasa yanamilikiwa na Wakulima.

Vile vile, madai ya Jussa kuwa ununuzi wa karafuu hufanywa na kampuni moja, hayana ukweli, kwani utaratibu ni kwamba, kunakuwa na ushindani wa zabuni, ambapo kampuni yenye bei ya juu hununua karafuu kupitia ZSTC.

Mbeto alizitaja Kampuni zilizonunua Karafuu ya Zanzibar ni Unit Trader ya India , Afcom Trading ya Dubai , Brookes Ltd ,KK Global Zenj Spice , Rkk ya India na Rho Traders African Afrika Kusini kinyume na madai ya Jussa aliiyedai karafuu ya huuziwa mtu mmoja.

“Kampuni tofauti toka nchi tofauti hununua Karafuu ya Zanzibar kupitia Shirika la SMZ la ZSTC. Kampuni yenye bei kubwa ndio inayopewa ruksa na Serikali inunue karafu Zanzibar,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here