Na Albert Kawogo
MADEREVA wanaotumia barabara ya Bagamoyo kuelekea mikoa ya Kaskazini ya Tanzania wametakiwa kuwa makini katika kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo na ulemavu wa kudumu.
Akizungumza katika zoezi maalum la ukaguzi wa magari na utoaji wa elimu kwa madereva hao, Mkuu wa usalama barabarani Bagamoyo, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi ASP Aziz Zuber amesema, wajibu wa kwanza wa dereva ni usalama wake na abiria watembea kwa miguu pamoja na vyombo vingine vya moto vilivyo barabarani.

ASP Zuberi amesema, ajali nyingi zinaweza kuepukwa ikiwa madereva watazingatia kanuni na wajibu wao wanapokuwa barabarani
Amesema wajibu huo ni pamoja na kuwa na leseni za chombo sahihi wanachokiendesha,kufuata sheria za barabarani, kutokutumia pombe au vilevi vingine kama bangi au mirungi.

Mkaguzi amesema, jukumu lao kama askari wa usalama barabarani ni kutoa elimu bila kuchoka lakini pia kuwaonyesha madereva hao kuwa jeshi la polisi haliko barabarani kwa ajili ya kutoa adhabu tu kwa madereva wazembe bali ni pamoja na kuwaelimisha kama sehemu ya kuwakumbusha wajibu wao ni kwa vipi wanapaswa ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Zaidi ya madereva 34 wa mabasi, malori na gari ndogo kwa nyakati tofauti barabarani walipewa elimu kuhusu sheria za usalama barabarani pamoja na kupimwa kwa kifaa maalum iwapo wametumia kilevi
Zoezi hilo limeelezwa ni endelevu na madereva wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi la polisi.