WAGOMBEA wa vyama vya siasa nchini wametakiwa kufuata sheria na miongozo ya kampeni ili kuepusha uchochezi na uvunjifu wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi, katika ukumbi wa Tume hiyo Maisara wakati akifungua mafunzo kwa wagombea wa majimbo na wanawake viti maalum.
Amesema kutofuata sheria na miongozo wakati wa kampeni kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani, hivyo wagombea wanapaswa kuzingatia maadili, haki na wajibu wao katika kampeni. Aidha, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na kuwaandaa kuelekea uchaguzi ili kila mgombea atambue sheria na kanuni zinazowaongoza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina, amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika, ikiwemo usambazaji wa vifaa vya uchaguzi katika wilaya zote, na kusisitiza kuwa tume imejipanga kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu uliopo.
Akizungumza katika mada ya umuhimu wa kudumisha amani, Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Shaaban Albataash, amewataka wagombea kutumia lugha ya staha katika kampeni, akibainisha kuwa lugha isiyofaa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Naye Mchungaji Timothy Phileman kutoka Kamati ya Amani Zanzibar amesema wabunge na wawakilishi wanapaswa kufuata sheria na sera zilizowekwa, kwani kutoziheshimu kunadhuru maisha ya wananchi.
Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Tume ya Uchaguzi kwa kuwapatia nyenzo muhimu za kuwaongoza katika kampeni, sambamba na kuitaka tume kusimamia vyema haki na wajibu wa wagombea wote.