Na Iddy Mkwama
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis ametaja mambo matatu ambayo yanakifanya Chama cha Mapinduzi (CCM) kiwe na uhakika wa kupata ushindi wa kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mbeto alitaja mambo hayo kwenye Mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar wakati akitangaza rasmi kuhusu tukio kubwa la uzinduzi wa kampeni za uchaguzi, linalotarajia kufanyika kesho, Septemba 13, 2025.
Kwanza, alisema kinachowafanya watembee kifua mbele, ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais Mwinyi kwa makundi mbalimbali Visiwani Zanzibar, sambamba na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Pili, CCM kina mgombea mzuri na tatu, chama hicho kikongwe kinaungwa mkono na wananchi wengi wa Zanzibar na wanakikubali kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Mbeto alisema, kutokana na kukubalika kwa chama hicho tawala na mgombea wake, ndio maana wameamua kufanya uzinduzi wa aina yake kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja, ni tofauti na wapinzani wao chama cha ACT Wazalendo ambao wamezindua kampeni zao ‘vichochoroni.’
“Sisi tupo Mnazi Mmoja na niwaambie, hawa wenzetu hawana mgombea anayeuzika. Tumeanza harakati za vyama vingi tangu mwaka 1995, Othman Masoud Othman (OMO) hajawahi kumuamini Maalim Seif Shariff Hamad, hajawahi kuamini hata harakati za upinzani, hajawahi kupiga kura,” alisema Mbeto.
Alisema, kwa hali hiyo wananchi hawawezi kumuamini Othman ambaye kwa miaka yote hajawahi kumpigia kura Maalim Seif. “Maneno haya si yangu, yamenukuliwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Thabit Idarusi Faina) wakati alipokwenda kujiandikisha Mpendae, alisema Othman ni mpiga kura mpya,”
Katika hatua nyingine, Mbeto alisema wamejiandaa vya kutosha kwa tukio la uzinduzi wa kampeni na hata Uchaguzi Mkuu, ambapo wana uhakika wa kuchukua viti vyote vya udiwani, uwakilishi na urais kwa asilimia 85.