SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeahidi kuendelea kutoa kila aina ya ushirikiano katika kuhakikisha programu ya tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), inayotarajiwa kuanza Januari 2026, inatekelezwa kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa zaidi kuliko awamu zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alitoa kauli hiyo alipokutana na watendaji wa TASAF kutoka Tanzania Bara na Zanzibar waliomtembelea ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa programu inayomalizika pamoja na mpango kazi wa awamu ijayo.
Mheshimiwa Hemed alisema, TASAF imekuwa chachu kubwa ya maendeleo na imewasaidia wananchi wengi nchini kujikwamua na umasikini kupitia ruzuku na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha, aliwataka watendaji wa TASAF kuendelea kutoa elimu kwa walengwa na wanufaika ili kuwaondoa kwenye mkanganyiko unaoweza kusababisha malalamiko kutokana na kutokuelewa vizuri masharti na taratibu za mpango huo.
“Ni muhimu walengwa wakapewa elimu ya kutosha kuhusu muda wa kuanza na kumalizika kwa programu, sifa za kunufaika na kikomo cha muda wa kupata huduma hizi ili kuepusha changamoto na malalamiko,” alisema Hemed.
Pia, aliwapongeza watendaji wa mfuko huo kwa moyo wa uzalendo na weledi wanaoonyesha katika kuhudumia wananchi licha ya changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais kwa ushirikiano na mshikamano anaouendeleza, akibainisha kuwa umechangia pakubwa mafanikio ya utekelezaji wa mfuko huo visiwani Zanzibar.
Ameeleza kuwa programu ya pili ya TASAF, inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2025, imefanikisha kuwafikia walengwa zaidi ya Milioni 1.3 Tanzania Bara na Zanzibar, huku zaidi ya Shilingi Bilioni 41.6 zikitumika kwa ajili ya ruzuku, ajira za muda na mitaji ya biashara ndogondogo.
Mziray alibainisha kuwa, programu ya tatu itajikita zaidi katika maeneo yaliyoathirika na umasikini na mabadiliko ya tabianchi, ambapo jumla ya walengwa 575,000 watanufaika kupitia ruzuku na ajira za muda.