Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imekamilisha ujenzi wa viwanja vya michezo vya Kitope, wilaya ya Kaskazini ‘B’.
Akizungumza na wanahabari viwanjani hapo, Mhandisi wa ujenzi wa viwanja hivyo, Geofrey Mabagala alisema, utahusisha viwanja jumuishi na kimoja cha soka.
Mabagala alisema, kiwanja kimoja kinaweza kutumiwa kwa michezo minne kwa nyakati tofauti ambayo ni mpira wa mikono, netiboli, wavu na kikapu.

Viwanja hivyo ambavyo ni sehemu ya programu ya Rais Dkt. Mwinyi ya kujenga viwanja 17 katika wilaya zote za Zanzibar, vina vyumba vya kubadilishia nguo, mabafu na cha marefa.
Mkazi wa Shehia ya Kitope, Idrissa Juma Hamduyni alisema, uwanja huo ni fursa muhimu kwa vijana wa eneo hilo katika kunoa na kukuza vipaji vyao na awali hawakutegemea kama wangeweza kuwa na viwanja vya namna hiyo.
“Viwanja vitawapa mwelekeo chanya vijana katika sekta ya michezo,” alisema mkazi huyo.