‘Hatutarajii kutumia nguvu kubwa kumnadi Dkt. Mwinyi Zanzibar’

0

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimesema, hakitarajii kutumia nguvu kubwa kumnadi Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari leo 20 Agosti 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, hali hiyo inatokana na kazi kubwa na nzuri aliyofanya Rais Hussein Mwinyi katika kipindi chake kuwatumikia waZanzibari.

“Utakuwa uchaguzi mwepesi sana na ushindi ni zaidi ya asilimia 75,” alisema mwenezi huyo na kuongeza kuwa, hakuna Shehia wala wilaya ambako hakuna alama yake.

Alisema, kulingana na ratiba ya Tume Huru ya Uchaguzi, kutangaza Agosti 28, 2025 kuwa ndio siku ya kuanza kuchukua fomu za Urais na Ubunge, siku ya Dkt. Mwinyi kwenda kuchukua fomu chama kitaitangaza na kinatarajia waZanzibari wengi kujitokeza kumsindikiza.

“Amefanyakazi nzuri, Zanzibar nzima itasimama kwa muda,” alisema.

Alibainisha kuwa, jinsi watakavyo fanya kampeni, idadi ya mikutano na taratibu zingine vitawekwa wazi baada vikao vya kikatiba vya CCM, Taifa vya kutangaza majina ya wagombea Ubunge na Wawakilishi wa chama hicho, vinavyoanza Dodoma Agosti 21, 2025.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here