Serikali yaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia

0

OR- TAMISEMI, Tabora

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Atupele Mwambene, amesema Serikali kupitia miradi mbalimbali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kuyafanya kuwa salama, bora na rafiki kwa walimu na wanafunzi ili kuinua kiwango cha elimu nchini.

Mwambene amezungumza hayo wakati akifunga mafunzo ya Walimu wa Ushauri, Unasihi na Ulinzi wa Watoto wa Shule za Msingi kupitia mpango wa Shule Salama unaotekelezwa chini ya Mradi wa BOOST, yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu mkoani Tabora.

Amebainisha kuwa Serikali imefanikisha ujenzi wa shule mpya 2,441 zikiwemo shule za msingi 1,399 na sekondari 1,042, hususani katika maeneo ya vijijini yaliyokuwa hayana shule au yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Aidha, jumla ya shule kongwe 906 zimekarabatiwa pamoja na miundombinu mingine muhimu ikiwemo vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni, mabwalo, maabara na maktaba.

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika kipindi cha mwaka 2022/23 hadi 2024/25 imepeleka jumla ya Shilingi Bilioni 539.6 shuleni na kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 656 za awali na msingi. Lengo kuu la uwekezaji huu ni kuhakikisha sisi kama Taifa, wazazi na walezi tunatoa fursa sawa kwa watoto wote kupata elimu,” alisema Mwambene.

Aidha, amewataka walimu na viongozi wa shule kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kwa kuweka masanduku ya maoni, kuanzisha mabaraza ya watoto pamoja na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni, huku wakihakikisha changamoto zinazowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa miongozo.

Vilevile, amewakumbusha walimu kote nchini kuzingatia nidhamu, maadili na miiko ya ualimu ili kuhakikisha wanafunzi wanatendewa haki na kulinda heshima ya taaluma hiyo kwa kuondoa kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here