Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, kuelewa kuwa siku zote mambo ya ngoswe huachiwa ngoswe mwenyewe, kwani yanayoendelea ndani ya CCM yanawahusu wana CCM wenyewe.
Chama hicho tawala kimemueleza Jussa atautambua ukweli wa mambo na kukubalika kwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ifikapo Oktoba Mwaka huu.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema matokeo ya Uchaguzi Mkuu ndio yatakayokata ngebe na kidomo domo cha Jussa.
Mbeto alisema, kwa miaka yote tokea 1995 hadi 2020, CUF baadae ACT, vilikuwa vikimsimamisha mgombea mmoja wa urais Hayati Maalim Seif Sharif Hamad na CCM hakikuwahi kuhoji.
Alisema, CCM hakikusema lolote au kuingilia matakwa ya demokrasia na maamuzi ya chama hicho wala kuhoji kwanini mgombea anakuwa mtu huyo, huyo miaka kwa miaka.
“Ni ajabu kumsikia Ian Smith wa Zanzibar akiingilia mambo ya CCM na kutaka Dkt. Mwinyi asiwe mgombea Urais Zanzibar. Tunaijua hofu alionayo Jussa na wenzake ni bidii, utayari na uchapakazi wa Rais Dkt. Mwinyi,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, kama kweli Jussa ni mwanademokrasia wa kweli ilikuwaje miongo yote hiyo ndani chama chao wawe na mgombea mmoja wa kudumu?
“Jussa anza kutoa boriti kwenye jicho lako kabla hujakitoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako. Maalim Seif amekuwa akigombea Urais kila mwaka hakuwahi kumkosoa. Mambo ya CCM huyawezi waachie waamue wana CCM wenyewe,” alisema Mbeto.
Pia, Katibu huyo Mwenezi amekitaka ACT kutoidanganya dunia kama mgombea wao wa Urais Zanzibar Othman Masoud Othman ana ubavu wa kumshinda Rais Dkt. Mwinyi.
Hata hivyo, Mbeto aliendelea kumkanya Jussa huku akimtaka kuacha siasa za jazba, uheke na udalali, badala yake awe mtu muungwana kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi na siasa
“Huyu Ian Smith wa Zanzibar hajui maana ya siasa yeye muda wote anahemkwa na chuki, gere na wivu wa jikoni. Aachane na siasa za Miaka ya 1950 wakati Zanzibar ikipigania uhuru. Siasa za ubaguzi na uhasama hazitakiwi tena Zanzibar na kizazi kipya,” alisisitiza.
Katibu huyo Mwenezi alisema, Jussa ameshiriki kuwafanyia mizengwe ili kuwazuia akina Juma Duni Haji na Mohamed Dedes wasigombee urais huku akimpigia debe Othman ili kulinda maslahi yake binafsi.