Vikosi vya SMZ kuendelea kuboreshewa maslahi

0

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali itaendeleza jitihada za kuboresha mazingira ya kazi kwa Vikosi vya SMZ, ikiwemo kuongeza maslahi ya wafanyakazi na kuboresha miundombinu ili kuongeza ari na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.

Hemed aliyasema hayo katika viwanja vya Chuo cha Mafunzo Hanyegwa Mchana, Wilaya ya Kati, wakati wa ufungaji wa Kozi ya Maafisa kwa Vikosi vya Zimamoto na Uokozi pamoja na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.

Aliwataka wahitimu hao kutoridhika na elimu waliyoipata, bali waendelee kujiongezea maarifa ya kijeshi na elimu ya kiraia ili kuwa watendaji wenye ufanisi mkubwa.

Aidha, aliwakumbusha kuwa kila Afisa wa vyombo vya ulinzi na usalama ana jukumu la kuhakikisha ulinzi na amani ya taifa inadumu.

“Mnapaswa kutunza haki, kujiepusha na rushwa, dharau, majivuno na kiburi katika maisha ya kila siku,” alisisitiza.

Akisoma risala, Afisa Msaidizi wa Chuo cha Mafunzo, Issa Chuom, aliomba chuo kipatiwe ndege ya bandia kwa mafunzo ya uokozi katika Chuo cha Mafunzo Kitogani, pamoja na kutengenezewa barabara za lami ndani ya maeneo ya vyuo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masuod Ali Mhammed, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada za kuleta maendeleo katika vyombo hivyo.

Akitoa taarifa ya kozi hiyo, Kamishna wa Chuo cha Mafunzo, CP Khamis Bakari Khamis, alisema jumla ya wapiganaji 154 wamehitimu, wakiwemo 85 kutoka Chuo cha Mafunzo na 69 kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokozi. Mbali na Kozi ya Uafisa, wahitimu walipatiwa pia mafunzo ya usalama barabarani, itifaki na mahusiano ya umma.

Katika kilele cha hafla hiyo, Hemed aliwatunuku vyeti wahitimu na kutoa zawadi kwa baadhi yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here