WANAFUNZI nchini wametakiwa kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwaingiza katika mazingira hatarishi yanayoweza kuhatarisha afya na mustakabali wao wa maisha.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Kitengo cha Uhamasishaji na Mabadiliko ya Tabia kutoka Programu Shirikishi ya Ukimwi, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma, Wizara ya Afya Zanzibar, Munaa Yussuf Mohamed, wakati akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Ufundi Mikunguni, Wilaya ya Mjini.
Munaa alisema, vijana wanapaswa kuwa waangalifu na makundi hatarishi yanayochangia kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), Homa ya Ini B na C, maradhi ya kujamiiana pamoja na ya ngozi.
Aidha, amewataka wananchi kuhamasisha vijana kupima afya mara kwa mara ili kuepuka changamoto za kiafya, ikiwemo maradhi ya afya ya akili ambayo yamekuwa yakiongezeka miongoni mwa vijana.
“Serikali inaendelea kuimarisha maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya na Miundombinu, ili kuwawezesha vijana kufikia maendeleo yao binafsi na ya kitaifa,” aliongeza Munaa.
Kwa upande wake, Daudi Kassim kutoka Taasisi ya Pamoja Youth Initiative, amewataka vijana kujiepusha na kushiriki kwenye vitendo vya vurugu vinavyochochewa na watu wasiopenda maendeleo.
“Vijana ni nguvu kazi na tegemeo la taifa. Ni wajibu wao kuwa wazalendo kwa kuijenga nchi yao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla,” alisema Daudi.
Baadhi ya vijana waliopatiwa elimu hiyo wamesema kuwa imewasaidia kupata mwanga juu ya namna ya kujilinda dhidi ya vishawishi vinavyoweza kuathiri maisha yao kwa sasa na baadaye.
Kongamano hilo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Vijana, na limeandaliwa na mashirika mbalimbali yakiwemo Youth Friends Service, Pamoja Youth Initiative, Zanzibar Integrated HIV, Hepatitis, TB and Leprosy Programme, kwa kushirikiana na Kituo Rafiki kwa Vijana – Mahonda, Rahaleo na KMKM.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa 2025 yanatarajiwa kufanyika Agosti 12, 2025, katika Skuli ya Utaani, Kisiwani Pemba, yakibeba kaulimbiu isemayo: