JUMUIYA ya Maradhi Yasiyoambukiza Zanzibar (NCDA) imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mkakati wake madhubuti wa kupima afya kwa jamii, ikiwa ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya maradhi yasiyoambukiza nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NCDA, Dkt. Said Gharib Bilal, wakati wa mkutano wa ushawishi, utetezi na kubadilishana uzoefu uliofanyika Mpendae, ukihusisha wadau mbalimbali kutoka ndani ya Jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza.
Dkt. Said alisema, mkakati huo wa Serikali utasaidia kugundua mapema magonjwa hatarishi kama shinikizo la damu, kisukari, saratani na maradhi ya moyo, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na kuchangia kwa kiasi kikubwa vifo visivyotarajiwa.
“Juhudi hizi za Serikali kupitia Wizara ya Afya ni za kupongezwa kwani zinasaidia wananchi kupata tiba mapema na kuokoa maisha yao,” alisema Dkt. Said.
Aidha, ameahidi kuwa NCDA itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu maradhi hayo na mbinu za kuyakabili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Louis H. Majaliwa, alisema ongezeko la maradhi yasiyoambukiza linatokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha na mtindo usiozingatia afya.
Ametoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kugundua matatizo mapema na kupata matibabu kwa wakati.
Naye Meneja wa NCDA, Haji Khamis Fundi, alisema kupitia mradi wa mkakati huo, jumuiya imeweza kuwafikia wadau mbalimbali kwa kuwaelimisha kuhusu maradhi hayo, wakiwemo waandishi wa habari, wasanii, watunga sera na watetezi wa haki za watu wanaoishi na kisukari.
Kwa upande wa watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza, wameishukuru Serikali kwa kujenga vituo vya afya vilivyosambaa katika maeneo mbalimbali, jambo lililorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.
Mkutano huo ulihusisha washiriki kutoka kada mbalimbali wakiwemo madaktari, waandishi wa habari, watu wanaoishi na maradhi hayo, pamoja na jumuiya wanachama, kwa lengo la kujadiliana mbinu bora za kuimarisha afya ya jamii.