Mbeto: Jussa na ACT yake wajiandae Kisaikolojia Oktoba 2025

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu kujiandaa Kisaikolojia, kwani chama chake hakitamudu mikikimikiki ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Kadhalika CCM kimemtaka Makamu huyo Mwenyekiti kuacha ngebe na kusambaza fitna ikiwa ni pamoja na madai kuwa kuna majimbo Rais Dkt. Hussein Mwinyi kaweka watu wake.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amemtaka Jussa na timu yake wajiandae kushuhudia matokeo yatokanayo na nguvu ya umma ifikapo Oktoba.

Mbeto alimtaka Jussa kuacha propaganda zilizopitwa na wakati huku akidhani atamudu kuwagawa WanaCCM kwa porojo zake, uzushi na fitna badala yake ametakiwa ajue kuwa muda umekwisha na sasa atashuhudia maamuzi ya haki yakipita.

Alisema, utendaji wa SMZ uliotokana na ubora wa Sera, Mipango na mikakati thabiti imetoa matokeo chanya, yenye tija na ufanisi na sasa hiyo ndio tiketi itakayomrudisha madarakani Rais wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi.

“Kila mcheza kwao hutunzwa. Kwa Maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi, wananachi wameapa kumrudisha madarakani na anamuombea Jussa Mungu azidi kumuweka hai aje akishuhudie kimbunga cha uchaguzi,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi, aliutaja ushindi wa CCM hautaki tochi, kwani kila mwananchi ameona kazi iliofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, miaka mitano iliyopita.

“Rais Dkt. Mwinyi amemaliza kazi ya kutumikia wananchi miaka mitano iliyopita. Jukumu pekee mbele yake ni kukamilisha kazi ya miaka mitano ijayo. Zanzibar itabadilika na kuwa Dubai, Thailand au Hong Kong ya Afrika Mashariki,” alieleza.

Alibainisha, madai ya Jussa kuwa Rais Dk Mwinyi ametuma wagombea majimboni, Mbeto aliwataka wanaCCM kupuuza porojo hizo za kitoto na kusema kazi ya kupandikiza wagombea ni ya Jussa na wenzake saba ndani ACT Wazalendo.

Mbeto alisema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Mwinyi walishatangaza hadharani wakiwa jijini Dodoma hawana mgombea yeyote aliyetumwa na viongozi hao kwenye jimbo lolote nchini.

“Dkt. Mwinyi hajamtuma mgombea yeyote. Kila mwana CCM aliyekwenda jimboni ameamua kwa utashi wake. Wajumbe ndio wenye maamuzi yupi apitishwe kwa mujibu wa sifa zake,” alieleza Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, Rais Dkt. Mwinyi mapema kabisa baada ya kuingia madarakani, aliikataa siasa za majibizano na malumbano majukwaani, akachagua kazi ya kutumikia wananchi na kujenga Zanzibar kimaendeleo.

Pia, Mwenezi huyo alimtaka Jussa aendelee na kazi ya kuwapa matumaini hewa wafuasi wake, lakini ukweli wa mambo utajulikana pale wananchi watakapopitisha maamuzi ya kidemomkrasia kwenye sanduku la kura Oktoba mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here