WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema Dira ya Maendeleo ya 2050 (Dira 2050) imekamilika na inatarajiwa kuzinduliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, jijini Dodoma.
Prof. Mkumbo alisema hayo leo, Julai 8, 2025 kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, ambapo alielezea hatua 13 ambazo mchakato wa dira hiyo imepitia na sasa umefika hatua ya 12, na inatarajia kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 na itabeba kauli mbiu ya ‘Tanzania Tuitakayo 2050.’

“Mchakato umekamilika, dira ya 2050 imekamilika na itatekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo,” alisema Prof. Mkumbo na kuongeza kuwa, Dira 2050 itaanza kutumika Julai 1, 2026.
Alisema, dira hiyo inatarajia kutekelezwa na Marais wa Awamu takribani mbili au tatu, na imekuwa tofauti na nyingine ambazo zimepita.
Prof. Mkumbo alisema, kupitia dira hiyo, Rais Dkt. Samia anaingia kwenye rekodi ya kuwa Rais wa Pili kuandaa dira ya Maendeleo; ya kwanza iliandaliwa na kuzinduliwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa.

Alisema, jambo la kipekee kwenye Dira 2050, haina mwelekeo wa Itikadi ya chama kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, huku akisisitiza, imewekewa ulinzi baada ya Rais Samia kuagiza ipelekwe bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, kuwekwa Azimio na kuidhinishwa.
Prof. Mkumbo alisema, lengo la kuipeleka dira hiyo bungeni, ni kuhakikisha kila Rais anayeingia madarakani, anaitekeleza na iwapo atataka kufanya mabadiliko, atalazimika kupeleka hoja bungeni na kulishawishi kufanya mabadiliko hayo.
Aidha, kwenye mkutano huo, wahariri wameishauri Serikali kutunga sheria maalumu kwa ajili ya kuilinda dira hiyo na kuwabana ambao hawataitekeleza, ushauri ambao ulipokewa na Prof. Mkumbo na kusema atauwasilisha Serikalini.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni mpango wa muda mrefu wa Tanzania unaolenga kuiongoza nchi kwenye mwelekeo wa uchumi wa kipato cha kati na juu ifikapo mwaka 2050.
Mpango huu, unalenga kukuza maendeleo endelevu, kuimarisha huduma, na kuongeza ustawi wa wananchi.