Na Edmund Salah, Kigoma
KAMISHNA wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi na kufanya kikao na Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Gombe na Milima ya Mahale zilizopo Kigoma.
Kikao ambacho kilijikita katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku.
Katika kikao hicho Kamishna Kuji alisisitiza bidii zaidi katika kufanya kazi, nidhamu na uadilifu na kubainisha kuwa mafanikio yanayopatikana katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni matokeo ya nidhamu, bidii, na uadilifu miongoni mwa Maafisa na Askari wa Uhifadhi katika kutekeleza majukumu ya Shirika.
“Nitoe pongezi zangu kwa mafanikio ambayo Shirika limeyafikia kwa mwaka huu utakaoisha tarehe 30 Juni, 2025 tumevuka malengo. Mpaka sasa Shirika limevuka malengo ya makusanyo ya mapato yaliyokusudiwa kukusanywa kwa mwaka wa fedha husika. Haya yote ni matokeo ya uadilifu, nidhamu na kujituma kwa kila mmoja wetu katika kutekeleza majukumu yetu” alisema Kamishna Kuji.
Akiwasilisha taarifa ya hifadhi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Yustin Njamasi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Gombe alimpongeza Kamishna wa Uhifadhi kwa kutenga muda wake na kwenda kuwatembelea kusikiliza na kujadili kwa pamoja mikakati ya namna bora ya kukuza uhifadhi na kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Pia, Kamishna Njamasi ameipongeza Bodi ya Wadhamini TANAPA pamoja na Menejimeti ya Shirika kwa namna ambavyo imekuwa ikiwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aidha, Kamishna Njamasi alimkabidhi Kamishna wa Uhifadhi tuzo ambayo ilitolewa kwa TANAPA kwa kuthamini mchango wa TANAPA katika kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi nchini iliyotolewa na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi Tanzania na kukabidhiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kassim Majaliwa.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Halid Mngofi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Mahale kwa mwaka fedha ujao imejidhatiti vilivyo katika kuhifadhi na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo pamoja mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Hifadhi ya Taifa Gombe na Milima ya Milima ya Mahale zilizopo Mkoani Kigoma zina umaarufu mkubwa unaotokana na uwepo wa idadi kubwa ya wanyama aina ya Sokwe Mtu.