SERIKALI imesema miradi 73 ya Biashara ya Kaboni imesajiliwa, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo tayari imeleta manufaa ya kiuchumi katika baadhi ya maeneo nchini huku Shilingi Bilioni 45 zimelipwa na kunufaisha wananchi katika halmashauri 10.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Bernadeta Mushashu aliyetaka kufahamu biashara ya kununua na kuuza kaboni imeinufaishaje Tanzania.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema miradi iliyosajiliwa ni ya sekta za misitu asilimia 51, nishati asilimia 33, taka asilimia tatu, kilimo asilimia nane na mifugo asilimia tano.
Akifafanua zaidi alisema, utekelezaji wa miradi hii huchangia katika uhifadhi na urejeshaji wa misitu na ardhi, kuongeza fursa za ajira na pato la wananchi kwa ujumla na kupunguza uzalishaji wa gesi joto hivyo kufikia malengo ya utekelezaji wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Khamis alisema, fedha zilizolipwa katika halmashauri 10 nchini hutumika katika kutekeleza miradi ya kijamii katika vijiji husika kama vile ujenzi wa shule, zahanati, malipo ya bima za afya, ada za shule na chakula kwa wanafunzi.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Bernadeta kuhusu vigezo vya kufanya biashara ya kaboni, Khamis alisema mwekezaji anatakiwa awe na kampuni ambayo ameisajili na kupata eneo kwa ajili ya upandaji wa miti.
Aliongeza kuwa, baada ya kupata eneo mwekezaji pamoja na ada ya usajili, anatakiwa aandae andiko na kuliwasilisha kwenye ofisi za Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro ili kupewa kibali cha utekelezaji wa mradi aliokusudia.