NHC na mikakati ya kuibadili miji na kujenga makazi bora

0

. Ni utekelezaji wa dhamira ya Rais Dkt. Samia

KWA takribani miaka mitano, miradi mbalimbali iliyokuwa inatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ilisimama, moja ya sababu kubwa zinazotajwa kukwamisha miradi hiyo, ni baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo kwenye nafasi zao.

Kwamba, walishindwa kuidhinisha upatikanaji wa fedha, lakini mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, aliruhusu NHC kukopa fedha kwa ajili ya kuiendeleza miradi hiyo ambayo mingine ni mikubwa na baada ya kukamilika, imekuwa msaada mkubwa kwa Shirika na hata kwa Serikali.

Kukwama kwa miradi hiyo kulisababisha baadhi ya wateja wao ambao wengine walilipia nyumba hizo kudai fedha zao, ambapo Shirika hilo liliwarudishia, ingawa wapo wachache walioomba fedha zao ziendelee kubaki, wakiamini miradi hiyo itaendelea.

Ndio kilichotokea, baada ya miaka kadhaa, miradi yote ikaendelea kwa kasi, bila shaka walioomba kurejeshewa fedha zao na kama hawakupata fursa ya kununua nyumba miradi ilipoanza tena, wanajutia maamuzi yao, huku wale waliokuwa na subra wakijipongeza na kufurahia uvumilivu wao.

Moja ya miradi ambayo ipo kwenye hatua za mwisho za ujenzi, ni Samia Housing Scheme (SHS) unaotekelezwa Kawe, jijini Dar es Salaam ambao ni ujenzi wa nyumba 500.

Mkurugenzi wa NHC Hamad Abdallah Hamad, anasema, nyumba hizo zote zimenunuliwa na zililipiwa mwaka mmoja uliopita, ambapo mwishoni mwa mwezi ujao, watakuwa wameshakabidhi nyumba hizo kwa wateja wao.

“Miradi mikubwa ilikwama, Rais wa Awamu ya Sita alipoingia madarakani, alitoa ruhusa ya kukopa kwa ajili ya kuendeleza miradi, ni kwasababu alitambua umuhimu wa miradi hii,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, mradi huo na mingine inatekelezwa kutokana na dhamira ya dhati ya Rais Samia ambaye anataka kuona miji inabadilika, lakini kubwa zaidi ni wananchi kupata makazi bora, na hilo NHC wanaendelea kulitekeleza kupitia kwa faida wanayoipata baada ya kuuza nyumba za gharama kubwa.

“Ile miradi unayoiona Makete na kwingineko, inatekelezwa baada ya kuwauzia watu nyumba za Milioni 500, 600, na soko lipo kwa hao wakubwa kwa maana ya kipato, hicho ndicho tunachokifanya,” anasema.

Anasema, Rais Samia aliwaelekeza kujenga nyumba za gharama nafuu, nao wapo kwenye hatua za mwisho za kupeleka andiko kwake kupitia kwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, ambaye atawasilisha kwa Rais andiko kuhusu namna ya kufikia kada za jinsi katika masuala ya nyumba.

“Rais anafuatilia kwa karibu sana, dhamira yake ni kuona miji yetu inabadilika, anataka kuona maboresho ambayo tutafanya kwenye nyumba zetu, lakini kikubwa zaidi anataka kuona watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, suala la kuwapatia wananchi makazi bora, ni suala kunwa duniani, kwani usipofanya vizuri kwenye makazi, kila siku utawakuta watu wako barabarani na ukiwauliza wanapotoka, watakutajia sehemu zenye makazi duni, ambapo watu wa aina hiyo hawana chakupoteza.

“Kwa mtu ambaye ana makazi bora hauwezi kumkuta anaandamana, kwasababu ametoka nyumbani ameacha familia, kukiwa na vurugu nyumba itaharibiwa, kwa hiyo namna pekee ya kutengeneza utulivu kwenye miji yetu, utulivu kwenye nchi yetu, ni kutoa makazi bora kwa wananchi,” anasema.

Mkurugenzi huyo aliongeza: “Katika nchi ambazo zimetoa makazi bora kwa wananchi, hauwezi kuwakuta barabarani, kwahiyo mheshimiwa rais analiangalia suala la makazi katika jicho tofauti.”

Mkurugenzi huyo anasema, kwa upande wao wanaamini ndio kipindi cha kufanya kazi kwa bidii, kwani kuna kiongozi ambaye anataka mabadiliko “ni fursa ambayo tunaitumia, kwasababu hiyo tunaenda kuanza Awamu ya Pili ya Samia House Scheme”

Aidha, Mkurugenzi huyo wa NHC alitaja baadhi ya miradi mikubwa ambayo ilisimama tangu 2018 na hivisasa inaendelea na mingine imekamilika, ni pamoja na Morocco Square ambao sasa umekamilika na nyumba zake 100 zimeuzwa kikamilifu; maeneo ya biashara na ofisi yamepangishwa kwa umma.

“Ufanisi huu umewezekana baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kutoa kibali cha kukopa Shilingi Bilioni 17 mwaka 2023 na kuukwamua mradi huu,” alifafanua Hamad Abdallah Hamad.

Mradi mwingine ni Kawe 711, anasema mradi huu wenye thamani ya Shilingi Bilioni 169 umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026. “Natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kupata kibali cha kukopa Shilingi Bilioni 174 mwaka 2023 fedha hizi zimesaidia kukamilisha mradi wa Morocco Square uliokuwa umesimama kwa miaka mitano na kuanza ujenzi wa Kawe 711.”

Pia, aliutaja mradi wa Golden Premier Residence (GPR) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 127 uliopo Kawe, kwasasa mazungumzo kati ya mkandarasi na Shirika yamekamilika na ujenzi unaendelea na utakamilika Septemba 2027.

Mwingine ni Plot 300, ambao upo eneo la Regent Estate, mradi huu nao ulikuwa umesimama kwa muda “Sasa tumeutangaza ili kupata mkandarasi wa kuendelea na ujenzi. Hatua hii inalenga kurejesha utekelezaji wa mradi huu uliokuwa umesimama tangu 2018 ili kuchochea maendeleo ya eneo la Regent Estate na jiji kwa ujumla.

Mbali na ukamilishaji wa miradi hiyo, anasema wanaendelea na mradi wa Awamu ya Pili wa SHS ambao ni nyumba za kuuza na maeneo ya biashara ya kupangisha, amapo asilimia asilimia 50 zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine.

“Mradi wa nyumba 5000 unaotekelezwa kwa Awamu, utagharimu Bilioni 466 sawa na dola za Kimarekani Milioni 200. Awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu umeanza eneo la Medeli, jijini Dodoma; Kawe na Kijichi jijini Dar es Salaam ambapo nyumba 908 zinajengwa,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, ujenzi wa nyumba 68 Iyumbu zimekamilika kwa asilimia 100, jengo la biashara Masasi (Mtwara) ujenzi umefika asilimia 75, jengo la biashara Morogoro (2H) umefikia asilimia 80, jengo la biashara Mtanda limefikia asilimia 54.

Miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa ni Mount Meru (Arusha), Tabora Commercial Complex (Tabora), Singida Shops (Singida), Kashozi Complex (Kagera); Mkwakwani Plaza (Tanga), Ulugulu Plaza (Morogoro), Iringa Commercial Complex (Iringa), Maghala ya biashara (Mtwara) na maduka ya biashara Ilala (Dar es Salaam) ujenzi wake umeanza.

Katika mwendelezo wa kujenga makazi bora na maeneo ya biashara, NHC wanatekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufungia uchumi wa nchi na kushirikisha sekta binafsi ambayo ni injini ya maendeleo endelevu ambapo Shirika lilifanya marekebisho ya Sera ya Ubia ambayo ilizinduliwa rasmi Novemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo wa NHC anasema, Sera hiyo imechochea ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa majengo ya matumizi mbalimbali ambapo jumla ya miradi 21 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 351 inaendelea kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam (17), Mwanza (3) na Iringa (1).

Kupitia sera hiyo ya ubia, shirika hilo limeidhinisha miradi mingine 64 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 607 na uchambuzi wa uwezo wa wawekezaji hao unaendelea kabla ya kupewa mikataba.

“Utekelezaji wa miradi hii una manufaa makubwa ikiwemo kuongeza upatikanaji wa nyumba bora za makazi na biashara kuongezeka kwa ajira kwa watanzania na kupendezesha mandhari ya miji yetu na wigo wa kodi na mapato ya Serikali,” anasema.

Akitolea mfano wa miradi inayotekelezwa kwa ubia, Mkurugenzi huyo anasema, eneo la Kariakoo kuna miradi 16 inaendelea ambayo inalenga kuvunja majengo ya zamani na kujayenga upya majengo ya makazi, biashara kwa maana ya maduka ambayo yatakuwa ya kisasa.

Anasema, ujenzi wa majengo hayo utaanzia chini ya ardhi, ambapo sehemu za maduka zitaishia ghorofa ya pili, na sehemu zitakazobaki ni makazi na wafanyabiashara watawekewa sehemu za kuhifadhia mizigo ambayo nayo itapandishwa kwa kutumia vifaa maalum.

“Ndani ya miaka mitatu ijayo, hakutakuwa na jengo la NHC la zamani Kariakoo, majengo yote yatakuwa mapya na yatakuwa na ghorofa 10 hadi 15, tayari tumeanza miradi 16, mingine 64 ipo njiani,” anasema Mkurugenzi wa NHC, Hamad Abdallah Hamad wakati akitoa wasilisho kuhusu utendaji wa Shirika hilo kwa Wahariri wa vyombo vya habari, Juni 16, 2025.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here