Nimesaini notisi ya kuvunja mabaraza ya madiwani – Mchengerwa

0

Na James Mwanamyoto OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa sheria, tayari amekwisha saini notisi za kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma.

Mchengerwa alisema, notisi hizo za kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya, na Mamlaka za Miji, 2025 zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali hivi karibuni.

Alifafanua kuwa, notisi hizo zinaelekeza kwamba vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa ziwe zimekoma siku saba kabla ya kuvunjwa kwa Bunge hapo Juni 27, 2025.

“Vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa kuwa zimekoma ifikapo tarehe 20 Juni, 2025 hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri atawajibika kwa kufanya kikao chochote cha Halmashauri au Kamati yake baada ya tarehe hiyo,” Waziri Mchengerwa alisisitiza.

Baada ya mabaraza ya madiwani kufikia ukomo Juni 20, 2025, Mchengerwa ameelekeza masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri kusimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiana na Wakuu wa Idara watakaokuwa kama wajumbe wa kamati.

Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa ameelekeza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hataruhusiwa kuanzisha miradi au uwekezaji mpya ikiwa ni pamoja na kubadilisha au kurekebisha mradi, uwekezaji au uamuzi wowote uliopitishwa na Halmashauri kabla ya kuvunjwa.

“Matumizi mabaya ya mamlaka au kutotekeleza kwa ufanisi majukumu ya kiutawala kwa mujibu wa notisi hizi, kutamfanya Mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa Sheria,” Mchengerwa amehimiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here