Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MSINGI wa elimu unatajwa kuanza utotoni na mtoto ili aweze kujifunza vizuri na kuwa na utulivu darasani, suala la miundombinu ya kisasa ya kujifunza na kufundishia inatajwa, lakini kubwa kuliko yote ni mlo; tena wenye lishe inayohitajika katika ukuaji wao.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na kujenga shule za kisasa zikiwemo za ghorofa zenye mahitaji yote muhimu katika kufundishia na kujifunza, anaenda mbali zaidi kwa kuamua kufanya uwekezaji wa lishe kwa watoto wote wa shule za awali Zanzibar.
Dkt. Mwinyi katika kukabili uandikishaji usioridhisha wa watoto wanaoanza shule za awali uliokuwepo miaka ya nyuma, anaamua kubuni mpango wa kuhakikisha watoto wote wa madarasa ya awali, wanapata Uji, Maziwa na Mkate wanapokuwa shuleni.
Mpango huo unatajwa kuchangia ongezeko la uandikishwaji watoto shuleni kutoka asilimia 60 mwaka 2020 hadi asilimia 89 mwaka 2024 na kiwango hicho; huenda kikaongezeka zaidi muhula mpya wa masomo 2026.
Katibu Mkuu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis anathibitisha kuwepo kwa mpango huo wa uji, maziwa na mikate shule za Awali.
Anasema, ni mpango huo ni ubunifu wa Rais Dkt. Mwinyi kuwafanya watoto wawe na utulivu na kuwasaidia, pia walimu kutimiza malengo yao kitaaluma kwa watoto hao.
“Watoto wote shule za awali wanakunywa maziwa, uji na mkate kila siku na wazazi hivi sasa hawalazimiki asubuhi kuwapa watoto wao mikebe ya vyakula kama awali,” anasema.
Anabainisha Mbeto kuwa, hali hiyo imechangia ongezeko la uandikishwaji wa watoto wanaoanza shule hali ambayo inasaidia kutimiza lengo la Serikali la kuhakikisha kila mtoto anayestahili, anaandikishwa na habaki nyumbani.
Anabainisha Mbeto kuwa, hakuna mtu asiyejua umuhimu wa maziwa katika ukuaji wa watoto na ndio maana hata wazazi wametambua hilo na kuwa na mwamko wa kwenda kuwaandikisha watoto shule.
Kukabili ongezeko hilo, shule mpya za kisasa za ghorofa za msingi na sekondari zimejengwa na ukarabati na marekebisho kwa zile za zamani ili kukabili ongezeko hilo na kuwafanya wasome wakiwa si zaidi ya 40 darasani.
Idadi ya wanafunzi darasani usiozidi kiwango hicho, anasema Mbeto kuwa ni takwa la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Anasema, mafanikio yanayoonekana sasa katika sekta zote Zanzibar na mwaka ujao wa fedha, maendeleo yatakuwa maradufu zaidi hususan katika elimu.
Kulingana na Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Shilingi Bilioni 864 zimetengwa kwa ajili ya vipaumblele mbalimbali vya wizara hivyo ikiwa ni asilimia 17 ya bajeti kuu ambayo Serikali imepanga kutumia.