Z’bar kuwa kituo bora cha utoaji huduma za usafiri wa anga

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inajipanga kuendelea kujenga miundombinu ya viwanja vya ndege ili kuiwezesha kuwa kituo bora cha utoaji wa huduma za usafiri wa anga.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua rasmi Mkutano wa Huduma za Usafiri wa Anga pamoja na Utalii Afrika, uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Ameeleza kuwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na ujenzi wa Uwanja wa Ndege mpya wa Pemba ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.

Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa hatua hiyo itaifungua Zanzibar kikanda na kimataifa kwa mashirika zaidi ya ndege kuja nchini, na hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea pamoja na kutangaza utalii wa Zanzibar.

Aidha, alisema huduma za usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa sekta ya utalii inayochangia asilimia 30 ya pato la taifa na kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.

Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya ndege ya kikanda na kimataifa ili kuongeza ufanisi na usalama katika viwanja vya ndege.

Vile vile, aliongeza kusema kuwa, katika miaka ya karibuni kumeshuhudiwa ukuaji mkubwa wa sekta ya utalii, uliotokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour iliyoitangaza Tanzania, ikiwemo Zanzibar, na kutambulika kwa vivutio vya utalii, utamaduni na urithi wa kihistoria.

Halikadhalika, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha huduma katika viwanja vya ndege, ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kupitia sera ya PPP, mashirika ya ndege ya kikanda na kimataifa, pamoja na kusimamia ipasavyo kanuni na miongozo ya huduma za usafiri wa anga na hali ya usalama wa nchi hatua inayochangia kuongezeka kwa mashirika ya ndege yanayotoa huduma nchini.

Mkutano huo wa Kimataifa wa Masuala ya Anga na Utalii, maarufu kama AviaDev Africa 2025, umejumuisha wawakilishi zaidi ya 530 kutoka sekta za anga na utalii, pamoja na mashirika 47 ya ndege kutoka Barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here