CCM: Tuna kazi ya kutumikia wananchi, si kutukana matusi majukwaani

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema viongozi wake wana kazi ya kufanya Siasa Safi na utekelezaji kwa vitendo kunakotokana na matakwa ya Sera zake na kutumikia wananchi bila kuwabagua.

Vile vile, chama hicho tawala kimejipambanua kuwa, ndio chama pekee Barani Afrika, kinachoheshimu heshima na utu wa kila binadamu.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akisema upinzani utaendelea kwa miaka mingi ijayo kupata tabu kushinda na sera za CCM.

Mbeto alisema, Siasa ya CCM na sera zake hazibaki ndani ya vitabu, kwenye makabati na katika mabango, bali hutekelezwa kwa vitendo ili kuleta maendeleo yanayoshuhudiwa hivi sasa Vijiji na Mijini.

Alisema, kuna vyama kadhaa Barani Afrika ambavyo ni hodari kwa kutunga Sera na kuandika Ilani za Uchaguzi lakini vinaposhika dola, hushindwa kutimiza wajibu kwa jamii.

“Siasa na Sera za CCM zinakwenda sambamba na utekezaji kwa vitendo ili kuleta msukumo chanya wa maendeleo. Wapinzani wetu ndipo wanapojikuta hawakubaliki kwa Wananchi,” alisema Mbeto.

Aidha, Mwenezi huyo alisema, siku zote kadri mtu akiitazama Tanzania; Bara au Visiwani, kumekuwa na hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na utekelezaji wa Sera za CCM.

“Watendaji wa Chama na Serikali za CCM kutwa kucha huchemsha bongo na kufanya mambo yasiende mrama. Kuchanua kwa maendeleo nchini ni uthubutu wa kubeba dhima na dhamana ya utekelezaji wa Sera,” alieleza.

Mbeto alisema, kwa sababu hiyo, ndio maana wananchi wanapohudhuria mikutano ya hadhara ya upinzani, huwasikiliza viongozi wao wanavyotoa matusi na jeuri kisha huwapuuza na kuondoka.

“ACT, Chadema, CHAUMA ,NCCR-MAGEUZI , Tadea na vingine magari yao yanapita katika barabara zilizojengwa na Serikali za CCM. Hata wanapoumwa hutubiwa kwenye hospitali zenye madaktari, dawa na vifaa tiba bora,” alisisitiza.

Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema, ndio maana viongozi wa upinzani, wanapokuwa majukwaani hukwepa kuzungumzia ushindani wa sera, badala yake wanatoa matusi, kejeli na kufanya siasa za ubaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here