Sera ya matibabu bila malipo yawafikia wagonjwa wa figo Zanzibar

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WANANCHI wataendelea kutibiwa bila malipo Zanzibar na mashine za kutosha za kusafisha figo bure zimefungwa Hospitali tatu kubwa, gharama ikibebwa na Serikali.

Mashine hizo na idadi yake kwenye mabano zimefungwa Hospitali ya Mnazi Mmoja (15), Mkoani Lumumba (10) na Hospitali ya Abdallah Mzee Pemba (8).

Pia, ujenzi umeanza wa Hospitali kubwa ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ambapo ikikamilika hakutakuwa na mgonjwa atakayesafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Hospitali zote za wilaya zimeboreshwa na zina uwezo wa kulaza wagonjwa hadi 200 kwa wakati mmoja zikiwa na vifaa na mashine za kisasa za X-Ray, Cit Scan, MRN, mashine za kutunzia watoto njiti, uzalishaji wa Oxygen kuwasaidia wagonjwa kupumua.

Vitanda vya kutosha vyenye mashine za kisasa vya wagonjwa mahututi na vifaa vingine.

Aidha, imeanzishwa kampuni kwa ajili ya kuhakikisha hakuna mgonjwa anayeandikiwa dawa akaikosa katika hospitali zote za Serikali sanjari na chakula; milo mitatu kwa siku kulingana na maelekezo ya madaktari kwa wanaolazwa kwenye hospitali hizo za serikali.

Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alibainisha hayo wakati akizungumza na wana habari kuhusiana na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM Zanzibar 2020-2025.

Mkutano huo ambao pia, ulihusu Ilani ijayo 2025-2030, Mbeto alisema katika sekta ya afya, Rais Dkt. Mwinyi ametekeleza chama kilivyoielekeza serikali na kupitiliza.

Alisema, utekelezaji wa serikali sekta ya afya umevuka hadi asilimia 300. “Ilani ya uchaguzi ilitaka serikali kujenga hospitali nne na mbili kufanyiwa marekebisho, Dkt. Mwinyi kajenga zingine sita, zikiwa na mashine za kisasa za uchunguzi wa afya na matibabu,”

Madaktari bingwa hivi sasa wapo 72 kutoka 20 waliokuwepo awali sanjari na wafanyakazi 4,500 kada ya afya wameajiriwa wakiwemo madaktari wa kutosha.

“Kana kwamba haitoshi, nyumba 82 za madaktari zinajengwa hospitali ya Mkoani zikiwa na kila kitu ndani kuanzia flat screen tv, friji, fenicha na vingine na pale anakuja yeye tu..” anabainisha Mbeto.

Hospitali kubwa ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, pesa imepatikana na ujenzi wake umeanza eneo la Binguni.

Kila baada ya kilometa 2 kuna kituo kidogo cha afya kutokana na 178 vilivyojengwa na Bima ya afya kwa kila MZanzibari inakuja.

Mbeto anabainisha kuwa bima ya afya ambayo itagharamiwa na serikali itampa uhuru mwananchi kutibiwa anakotaka hususan hospitali za watu binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here