CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030 waliyoizindua imebeba matumaini, kwani ina mambo muhimu yanayowagusa watanzania.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla ameeleza hayo leo Juni 5 wakati alipopita kusalimia wananchi katika eneo la Mto wa Mbu, wilayani Monduli, mkoani Arusha akiwa njiani kuelekea Karatu kwa ajili ya Mkutano wa hadhara akiendelea na ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Alisisitiza, ilani hiyo iliyozinduliwa imetokana na tathmini ya ilani iliyopita kwa kufanya utafiti na ushirikishwaji wa wananchi, asasi za kiraia na wadau mbalimbali ili kujua vipaumbele na mahitaji ya watanzania.
Makalla alisema, ilani hiyo inakwenda kushughulika na ajira, kuimarisha uchumi, miundombinu na changamoto zote zinazowakabili watanzania na muda utakapofika watainadi kwasababu ni ilani ya watanzania na inahusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
“Inaenda kushughulika na maisha ya watanzania kwahiyo ahadi yetu muda utakapofika tutakwenda kuinadi ilani hiyo ni ilani yenu ninyi ndo mustakabali wa maisha ya watanzania, kwani hakuna chama chenye Ilani nzuri zaidi ya CCM,” alisema Makalla.