MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko amesema kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ni dhahiri kwamba lengo la 80% ya wananchi kutumia nishati hiyo litafikiwa ifikapo Mwaka 2034.
Amesema hayo Agosti 15, 2025 wakati wa kutambulisha mradi wa kusambaza majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa jiko unaoratibiwa na REA na kutekelezwa na Mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited iliyoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo katika Mkoa wa Katavi.
“Tunaipongeza REA kwa kuja na mkakati huu na kutufikia hapa Mpimbwe, kwani licha ya kwamba sisi tupo katika mikoa ya pembezoni, kwa maana ya Mkoa wa Katavi, lakini ni mikoa ambayo imeweza kufikiwa; wananchi wameifurahia huduma ya majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 19,500 tu,” alisema Mwariko.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inaningia, inasimamia na inaishi katika mazingira ya Nishati Safi.
“Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sio tu kwasababu amekuwa kinara lakini tunamshukuru kwakuwa ameweka mifumo, miundombinu, misingi na mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kweli nchi yetu inafikia kuwa nchi yenye kutumia nishati safi, nishati bora na ya kisasa,” alisema Mwariko.
Alibainisha kuwa Halmashauri ya Mpimbwe tayari imeanza uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa taasisi zinazotoa huduma ya chakula kwa watu wake zikiwemo shule za msingi na sekondari na kwamba baadhi ya shule ikiwemo shule ya Sekondari Mizengo Pinda tayari imefungiwa mfumo wa Nishati Safi ya Kupikia.

“Hivi tunavyozungumza tayari ofisi za walimu zote za shule za msingi na sekondari wanayo majiko ya gesi kwa ajili ya kuhakikisha wanatumia nishati kupika chakula; kwahiyo kazi iliyopo hapa ni kuhakikisha hata mwananchi wa ngazi ya chini kabisa anaona umuhimu wa utumiaji wa huduma hii na anaitumia bila ya kurudi nyuma,” alibainisha Mwariko.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majimoto, Seltus Mwanampemba alisema tunayo haja ya kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwani matumizi ya gesi yanasaidia kuokoa gharama mfano unapotumia mkaa kama ulitaka kuchemsha kikombe cha maji ule mkaa ndio umeupoteza maana yake unatumia gharama kubwa kwa kazi ndogo.
Alisema, kumekuwa na mtazamo hasi kwa badhi ya watu kwamba ladha ya chakula inabadilika kwa kutumia nishati safi kupikia jambo ambalo alisema halina ukweli na alitoa wito kwa jamii kuondokana na mtazamo huo kwani yeye anatumia nishati safi kupikia na ladha ya chakula ni ile ile kama wakati ule aliyokuwa akitumia kuni.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Majimoto, Dakson Schula alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha shule hiyo kupata nishati safi ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi.
“Tunamshukuru Rais Samia, shuleni kwetu tumepata nishati safi ya umeme lakini pia kuna mfumo wa jiko la gesi unajengwa ambao utasaidia kupikia shuleni kwani kwa utaratibu wa hapa shule huwa tunapata chakula,” alishukuru Schula.
Kwa upande wao wananchi walionufaika na majiko ya ruzuku wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kununua majiko walipongeza hatua inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha wanananchi wa kipato cha chini nao wanafikiwa na wanabadilishiwa maisha yao.

“Tulikuwa tukitumia mkaa na kuni kupikia lakini sasa tunamshukuru Rai Samia na hii kampeni yake ya Nishati Safi kwa wote, katuona akina mama, katusaidia kuondokana na kuni na mkaa; baadhi yetu hatukuwa na uwezo wa kununua majiko ya gesi lakini sasa kwa ruzuku hii kila mmoja atakuwa na jiko la gesi nyumbani kwake,” alisema Editha Kabagi, Mkazi wa Mpimbwe.
“Hakika Rais Samia ni Mama, ana uchungu, ametuonea huruma wamama wenzake, kwakweli tumefarijika kwani tulikuwa tunapata shida lakini sasa hali inakwenda kubadilika,” alipongeza Aportuna Simmi, mkazi wa Mpimbwe.
Akizungumza kuhusiana na zoezi hilo la usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku, Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali alisema, mwitikio wa wananchi ni mkubwa na hilo linadhihirisha kuwa wanadhamira ya dhati kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ambazo sio safi na salama na kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi.

Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo hasa ikizingatiwa kuwa faida za kutumia Nishati Safi ya Kupikia ni nyingi ikiwemo kulinda afya na kuokoa mazingira.
Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatumia njia mbalimbali katika kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha wananchi ili kufikia lengo la 80% ya wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo Mwaka 2034.
