WAKANDARASI wa ndani (wazawa) sasa wanapata kwa urahisi ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa wakati na kwa ufanisi.
Mtaji huo wanaupata kupitia hatifungani maalum iliyoanzishwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB.
Hatifungani hio ya kwanza katika sekta ya miundombinu nchini lengo lake ni kuwezesha utekelezaji wa miradi ya barabara vijijini na mijini kupitia ushiriki wa wakandarasi wazawa.
Jina lake ni Samia Infrastructure Bond, ilizinduliwa rasmi Novemba 29, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Mhasibu Mkuu wa TARURA, CPA Jacob Nyaulingo, amesema katika mahojiano haya maalum kwamba,
Wazo la kuanzisha hatifungani hiyo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
“Awali lengo lilikuwa ni kukusanya shilingi bilioni 150 lakini kutokana na mwitikio mkubwa kutoka kwa watanzania wa kuunga mkono juhudi hizi hali iliyopelekea kuvuka lengo hilo la ukusanyaji kutoka bilioni 150 hadi kufikia shilingi bilioni 323 sawa na asilimia 215.4 ya matarajio,” amesema.
Hatifungani hiyo ina riba ya asilimia 12 kwa mwaka na fedha zilizopatikana zimeelekezwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya barabara chini ya TARURA.
“Ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinawafikia wakandarasi kwa haraka na bila urasimu, mfumo maalum wa kidijitali uitwao Samia Infrastructure Portal umeanzishwa,” amesema.
Ameongeza “Portal hiyo, iliyoundwa na TARURA kwa kushirikiana na CRDB, inawawezesha wakandarasi kuwasilisha maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao.
“Mfumo huu huondoa usumbufu wa kusafiri na kusaini nyaraka katika ofisi mbalimbali za TARURA na benki.
“Badala yake, wakandarasi hujaza maombi mtandaoni, ambayo hupelekwa moja kwa moja TARURA mkoa kwa ajili ya uhakiki kabla ya kutumwa CRDB kwa hatua za mwisho za kifedha,”.
Kwa mujibu wa CPA Nyaulingo, mfumo huu umeandaliwa kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwazi katika mchakato wa mikopo.
Amesema miongoni mwa bidhaa zinazopatikana kupitia mfumo huu ni pamoja na Bid Guarantee, Performance Guarantee, Advance Payment Guarantee, Retention Guarantee, Certificate Discounting na huduma mpya kabisa ya Bridge Financing, inayolenga kumpatia mkandarasi mtaji wa haraka kabla ya malipo ya mkataba.
Katika hatua ya kuwezesha wakandarasi zaidi, CRDB imeamua kutoa mikopo hiyo bila dhamana, huku ikitoza riba nafuu chini ya asilimia 15 kwa mwaka kwa wakandarasi wanaolipa kwa wakati.
“Tunatoa wito kwa wakandarasi wote nchini kutumia fursa hii adhimu. Ni wakati wa kutekeleza miradi ya barabara kwa ufanisi, kwa wakati, na kwa kutumia teknolojia bora inayowezesha upatikanaji wa fedha kwa haraka”.
“Kupitia mfumo huu, tunaamini kuwa sekta ya miundombinu itapiga hatua kubwa na kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” amesema CPA Nyaulingo.
Amesisitiza mpango huu wa hatifungani unadhihirisha dhamira ya serikali katika kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kuharakisha maendeleo ya barabara na kuinua kipato cha wazawa kupitia fursa halisi za utekelezaji wa miradi ya kimkakati.