‘𝑨𝒅𝒗𝒆𝒏𝒕𝒖𝒓𝒆 𝑹𝒂𝒄𝒆’ 𝒚𝒂𝒗𝒖𝒕𝒊𝒂, 𝒚𝒂𝒛𝒊𝒅𝒊 𝒌𝒖𝒆𝒍𝒆𝒌𝒆𝒂 𝒌𝒊𝒎𝒂𝒕𝒂𝒊𝒇𝒂

0

Na Mwandishi Wetu, Arusha

MASHINDANO ya Meru Forest Adventure Race 2025 yamefanyika Agosti 31, 2025, katika Hifadhi ya Shamba la Miti Meru/USA, yakihudhuriwa na mamia ya washiriki kutoka ndani na nje ya mkoa wa Arusha.

Tukio hilo lilizinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi, ambaye pia alishiriki mbio za Kilomita 10 za msituni.

Akizungumza baada ya kumaliza mbio, Mwinyi alisema tukio hilo limechangamsha washiriki kimwili, limeimarisha mshikamano wa kijamii na kuongeza thamani ya utalii wa misitu.

“Ni mbio za kipekee ambazo zimenikutanisha na watu wengi. Changamoto za msitu, maporomoko ya maji na mandhari ya asili yameongeza furaha na msisimko kwa washiriki. Niwapongeze TFS na waandaaji kwa kuendeleza falsafa ya utalii wa michezo inayosisitizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwinyi.

Kwa upande wake, Xavery Thobias Chuwa wa Quality Sports Promoters alisema mwaka huu wameanzisha Obstacle Race yenye changamoto za viwango vya kimataifa, ikiwapa washiriki uzoefu wa kipekee na kuvutia wageni kuja kutalii ndani ya msitu.

Tukio la leo lilijumuisha michezo ya kuvutia na burudani mbalimbali. Washiriki walishindana katika mbio za kilomita 5, 10 na 20, huku Enduro kwa pikipiki ikihusisha wanafunzi, wa kati (Intermediate) na wataalamu (Professionals). Baiskeli na motocross zilichangia msisimko, na washindi walipewa zawadi maalumu.

Aidha, tukio lilipambwa na burudani za kitamaduni, ikiwa ni pamoja na ngoma za Maasai, nyamapori choma na vinywaji vya aina zote, zikichangia hali ya sherehe na furaha kwa washiriki na wageni.

Afisa Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Yusuf Tango, alisema lengo ni kukuza utalii wa ikolojia na michezo. Mhifadhi Mkuu, PCO Ali D. Maggid, alibainisha mpango wa kutanua mashindano hayo hadi kimataifa, ili kuongeza idadi ya washiriki na kutangaza hifadhi za Tanzania kama vivutio bora vya michezo na utalii wa asili.

Meru Forest Adventure Race, ambayo inaingia msimu wake wa tatu mwaka huu, inatarajiwa kuchochea utalii wa michezo na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here