ZIFF yapitisha Filamu 70, kufanyika Agosti

0

Na Andrew Chale, Dar es Salaam

TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi Zanzibar maarufu kama ZIFF (Zanzibar International Film Festival,) wamepitisha filamu 70 kati ya 3000 zilizowasilishwa ambazo zitashiriki katika kuwania tuzo za ZIFF kwa msimu wa 27, 2024 utakaofanyika Agosti 1 hadi 4 Visiwani Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari, Julai 16, 2025, katika kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut,) wakati wa utangazaji wa filamu zilizotinga katika kinyang’anyiro hicho, Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF Hatibu Madudu alisema, kwa mwaka huu filamu zaidi ya 3000 zilikusanywa kutoka nchi zaidi ya 100 na mabara yote ulimwenguni.

Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF Hatibu Madudu

Alisema, Filamu 70 zilizoingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hizo ni pamoja na filamu bora ndefu, filamu bora Makala, tuzo maalum ya Emerson’s ambayo inatolewa kwa filamu bora kwa upande wa Zanzibar, filamu bora fupi, filamu bora ya hali halisi na filamu bora Afrika Mashariki.

Nyingine ni muigizaji bora Afrika Mashariki wa kike na kiume, Muigizaji bora wa kike na kiume Tanzania, Tuzo maalum ya Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambayo hutolewa kwa waandaaji wa filamu wawili, tuzo ya maisha katika Sanaa, na kwa pekee mwaka huu, kuna kipengele kipya cha chaguo la watu itakayoleta msisimko katika soko la Tamthilia.

“Kuna jumla ya filamu ndefu 25, Makala 13, Thamthilia10, filamu fupi 22…Kuna viwango vikubwa na ubora katika kazi hizi na zoezi la kupiga kura litaanza tarehe 20 mwezi huu hadi tarehe 3 mwezi ujao, hivyo waandaaji na waigizaji watengeneze mikakati ya kupigia debe kazi zao ili ziweze kushinda.” alisema.

Kuhusu uwasilishaji wa Filamu za Tanzania Madudu alisema, watayarishaji wamejitokeza kwa wingi na kwa miaka mitatu mfululizo, Filamu za Tanzania zimekuwa zikishinda tuzo hizo za Kimataifa na kuwataka kuwasilisha filamu nyingi zaidi.

Alisema, katika tamasha hilo kutakuwa na ‘Zanzibar Day’ itakayofanyika Julai 31 mwaka huu, ambapo burudani na filamu mbalimbali kutoka Zanzibar ikiwemo ‘House of Wonders’ zitaoneshwa na hiyo ni pamoja na ‘Workshop 11’ zitakazohusisha mafunzo ya filamu, utengenezaji filamu kwa kutumia simu pamoja na namna ya kukuza sekta ya Sanaa kwa ujumla.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini Tanzania Ms. Christine Grau alisema, kauli mbiu ya mwaka huu ya Rejuvenation ‘Kuhuisha’ ambayo imewalenga vijana, ni moja ya kipaumbele kikubwa cha EU katika kuwawezesha vijana katika nyanja mbalimbali ikiwemo Sanaa na wataendelea kushirikiana katika tamasha hilo.

Ms. Christine ameeleza kuwa, EU itaendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za sanaa na jamii kupitia miradi mbalimbali ambayo tayari inaendelea ikiwemo ya kuwawezesha wanawake.

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini Tanzania Ms. Christine Grau

Naye Mkurugenzi wa ZIFF, Joseph Mwale alisema tamasha hilo lina lengo la kuongeza uelewa wa tasnia ya filamu na kukuza Sanaa ya majahazi ya Bahari ya Hindi ikiwemo Asia ya Kusini, Mashariki, Rasi ya Uarabuni, Ghuba ya Uajemi, Iran, Pakistan, India na visiwa vya Bahari ya Hindi.

“Tamasha litakuwa na majukwaa mbalimbali ikiwemo jukwaa la watoto, wanawake wa vijijini, mbio za ngalawa, mpira wa miguu ufukweni kwa wanawake, majadiliano pamoja na uoneshaji wa filamu za kuvutia za Zanzibar. alisema.

Mkurugenzi wa ZIFF, Joseph Mwale

Alisema, tamasha hilo linatarajiwa kuwa na watazamaji takribani 2000 kwa kauli mbiu ya Rejuvenation ‘Kuhuisha’ ambapo filamu 3000 zilipokelewa kutoka maeneo mbalimbali duniani zikiwemo (Tanzania 62, Uganda 123, Kenya 169, Rwanda 12, Burundi 3 na Afrika Kusini 71,) huku filamu nyingine zikitoka katika Mataifa zaidi ya 100 ikiwemo Ujerumani, China, India, Somali, Ghana, Denmark, Senegal, Jamhuri ya Korea, Urusi, Ukaraine, Indonesia, Poland na Uingereza.

Mwale alisema, kwa mwaka 2024 Tamasha hilo limebebwa na kauli mbiu ya Uhuishaji wa masuala mbalimbali ambayo yalionekana kusuasua na kwa mwaka huu mambo mapya yameongezwa ikiwemo ushiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Vijana wa Vyombo vya Habari (IYMS,) ambao wataleta vijana 100 kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Vijana hao watafanya filamu fupi kwa lengo kuhamasisha vijana kote ulimwenguni kutumia filamu na vyombo vya habari kuhamasisha, kuelimisha na kuendesha hatua za masuala muhimu ya kimataifa.

Katika Tamasha hilo Thamthilia zinazowania tuzo ni pamoja na Ripoti, Bunji, Dhohar, Twisted, na Juakali, huku filamu zikiwa ni pamoja na Gwiji wa Taarab, ‘Zanzibar Untold,’ Unbankable na nyingine nyingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here