‘Ziara ya Korea imekuwa na mafanikio makubwa’

0

WAZIRI Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema ziara yake ya kikazi Nchini Korea imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa malengo aliyokuwa amejiwekea kwa asilimia kubwa yamefanikiwa.

Kuanzia Machi 9, 2025 Waziri Masauni alifanya ziara ya kikazi nchini humo akiambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali kuhusu Biashara ya Kaboni.

Alisema, suala hili ni mtambuka na geni hapa nchini na bado linahitaji uelewa na uzoefu wa kina kutoka nchi zilizoendelea katika kusimamia suala hili ili kuwezesha usimamizi madhubuti kwa nchi kwenye biashara ya kaboni.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa zikileta madhara mengi kama vile mafuriko, hali ya hewa isiyotabilika, ukame pamoja na maeneo ya maji safi kuingia chumvi jambo ambalo limekuwa likiathiri Maisha ya kibinadamu kwa njia moja na nyingine.

Alisema, athari hizo husababishwa na gesi joto inayotapataa katika anga ambapo chanzo chake kikubwa ni shughuli za maendeleo za uchumi za kibinadamu hasa katika shughuli zinazofanyika kawenye viwanda na Tanzania ni miongoni mwa wahanga kutokana na shughuli hizo zinazofanywa na mataifa yaliyoendelea.

Aliongeza, mbali na athari hizo lakini Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kupunguza gesi joto ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa wananchi, kulinda na kutunza mazingira ikiwa sambamba na kuhamasisha upandaji wa miti katika maeneo yaliyokuwa wazi.

Masauni alisema, kumekuwa na miradi mingi ambayo inafanyika nchini kupitia waizara mbalimbali ambayo kwa kutumia teknolojia inayopunguza matumizi yanayotoa gesi joto nyingi na kusababisha athari na hiyo imefanyika kwa miaka mingi bila kuona mabadiliko.

Masuala ya Biashara ya Kaboni hapa nchini yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR) kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kilichopo mkonai Morogoro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here