KATIKA kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mto Ruvu, Shirika lisilo la Kiserikali la WWF limekabidhi miche 2,500 ya michikichi kwa vikundi vya kijamii katika vijiji vya Mwembengozi, Kimaramisale na Kitomondo Ruvu, Halmashauri Wilaya ya Kibaha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Evelyne Ngwira, aliwashukuru WWF na Bodi ya Maji Bonde la Ruvu kwa ushirikiano wao katika kutekeleza mradi huo wa kilimo hifadhi.
Alieleza kuwa hadi sasa zaidi ya ekari tano zimepandwa michikichi na kusisitiza matumizi ya wataalamu wa kilimo kwa tija ya zao hilo.
Ngwira alisema, michikichi husaidia kuhifadhi mazingira, huku pia ikiwa chanzo cha mafuta, sabuni, kuni na kipato kwa familia.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Afisa Tarafa wa Ruvu, Roina Ilomo, aliwataka wanavikundi kuhakikisha miche inatunzwa ipasavyo ili kufikia malengo ya mradi.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi kutoka WWF, Eng. John Kasambili, miche hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mafunzo ya utunzaji mazingira yaliyotolewa kwa wanavikundi.
Mradi huu ni sehemu ya Mradi wa Usalama wa Maji kwa Jiji la Dar es Salaam na Mijiji ya Pembezo, unaofadhiliwa na kampuni ya ABInBeV/TBL, uliyozinduliwa mwaka 2022 na Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi.
Kupitia mradi huo, tayari miche 2,200 imepandwa katika vijiji vya Ruvu Station, Minazimikinda na Kitomondo; mizinga 45 na miche rafiki wa maji 20,000 imetolewa kwa vijiji 9 vya Kibaha na Kisarawe, sambamba na ujenzi wa miundombinu ya maji na uboreshaji wa takwimu za ubora wa maji ya Mto Ruvu.
Aidha, ukarabati wa bwawa la Kiembaemba unatarajiwa kuanza Julai 2025.