WMA yaunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa Jeshi la Polisi

0
Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa kivipimo Ilala, Muhono Nashon, akikabidhi Kichapishi kwa Kamishna Msaidizi wa Polisi na Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala Mohammed Makusi, katika hafla ya WMA kukabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Jeshi la Polisi Ilala iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salaam, Septemba 10, 2024.

Na Mahamudu Jamal, WMA

WAKALA wa Vipimo (WMA) imekabidhi msaada wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Ilala, Septemba 10, 2024 katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam.

Akiongoza makabidhiano hayo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Meneja wa Mkoa wa kivipimo Ilala Muhono Nashon alisema, msaada huo ni kutokana na ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya kazi baina ya WMA na Jeshi la Polisi hususani katika masuala ya jinai, ulinzi na usalama kwa maeneo mbalimbali ya ukaguzi, na nyanja nyinginezo.

Meneja Muhono amebainisha kuwa ushirikiano huo baina ya WMA na Jeshi la Polisi umekuwa na tija kutokana na Jeshi hilo kudumisha hali ya amani na usalama kwa watumishi wa WMA na wananchi kwa ujumla katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Aidha, aliongeza kuwa, WMA imekabidhi vifaa hivyo ili kuunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi.

“Vifaa hivi vitatumiwa na Jeshi letu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na ni matumaini yetu kuwa vitaongeza ufanisi katika utendaji wake,” alisema Nashon.

Kwa Upande wake Kamishna Msaidizi wa Polisi na Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala Mohammed Makusi, ameishukuru WMA kwa msaada huo na kusisitiza kuwa Jeshi hilo litaendelea kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

“Vifaa hivi vimekuja wakati muafaka, tukielekea katika Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania ambayo yatafikia kilele chake tarehe 27, Septemba, 2024”

Alisema, Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni Huduma bora za kipolisi zitapatikana kwa kubadili fikra, usimamizi wa sheria na matumizi ya TEHAMA.

“WMA mmetuunga mkono katika TEHAMA, hivyo tunawashukuru kwa hiki mlichotupatia ambacho kitasaidia kuboresha huduma zetu,” alisisitiza Kamishna Msaidizi Makusi.

WMA imekuwa na utaratibu endelevu wa kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi kwa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Vipimo, ushauri wa kitaalamu, semina elekezi na uwezeshaji kwa baadhi ya Taasisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here