WMA yataja mafanikio na mwelekeo wake ndani ya uongozi wa Awamu ya Sita

0

WAKALA wa Vipimo (WMA) umetaja mafanikio kadhaa ambayo yamepatikana kwa kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Machi 25, 2025, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA Alban Kuhulla alisema, miongoni mwa mafanikio hayo ni kuhakiki vipimo 3,668,149 vitumikavyo katika sekta mbalimbali nchini kati ya vipimo 3,923,652 ilivyopanga kuhakiki ambayo ni sawa na asilimia 94 ya lengo.

“Kati ya vipimo hivyo vilivyohakikiwa, vipimo 102,969 vilikutwa na mapungufu ambayo yalirekebishwa na kuruhusiwa kuendelea kutumika na vipimo 5,607 vilikataliwa kutumika baada ya kuonekana na mapungufu ambayo hayarekebishiki.” alisema Kihulla.

Aliendelea kusema: “Wakala inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuiwezesha kupata ajira za watumishi 186 wa kada ya ukaguzi wa vipimo ambao wataongeza nguvu kwenye jukumu la uhakiki na ukaguzi wa vipimo hapa nchini.”

Mafanikio mengine ambayo WMA wameyapata, ni kujenga majengo mapya ya ofisi katika Mkoa wa Mara na Simiyu. Vile vile, ujenzi wa ofisi hizo umefanyika katika Mkoa wa Dodoma, ambapo ujenzi wa jengo ambalo sasa linatumika kama ofisi za Wakala wa Vipimo Makao Makuu ulikamilika Machi, 2025 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.99.

Pia, WMA imeendelea kununua vifaa vya kitaalam kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo Iron Weight 500kg (100) kwa ajili ya kufanyia uhakiki na ukaguzi wa mizani kubwa zinazotumika viwandani na kwenye barabara na mitambo mikubwa miwili na mitambo midogo 10 inayobebeka kwa ajili uhakiki dira za maji.

Alisema, Wakala wa Vipimo imenunua mitambo 12 kwa ajili ya kuhakiki vipima mwendo kwenye vyombo vya usafiri, kati ya mitambo hiyo, mitambo 10 inabebeka ambayo itasambazwa kwenye mikoa.

“WMA imenunua mitambo miwili ya kusimika ambapo mtambo mmoja unaendelea kusimikwa katika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu na mtambo mwingine utasimikwa katika ofisi ya Makao Makuu Dodoma,”

“Wakala imenunua mita nne za mtiririko kwa ajili ya kuhakiki mita zilizofungwa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta, migodini, viwanja vya ndege na sehemu nyingine zinazotumika kujaza mafuta kwa kasi kubwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa mita hizo zinatoa vipimo sahihi vya kiasi cha mafuta,” alisema.

Mbali na ununuzi wa vifaa hivyo, Kihulla alisema kuanzia mwaka 2021/22 hadi Februari, 2025, Wakala imechangia jumla ya Shilingi Bilioni 17.1.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wakala inatarajia kuchangia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali zaidi ya Shilingi Bilioni 7 ambapo kufikia Februari, 2025, Wakala imechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 3.8,” alisema.

Kihulla alisema WMA pia, imefanikiwa kuhakiki idadi kubwa ya matenki ya magari yabebayo vimiminika shughuli ambayo inafanywa kupitia kituo kikubwa cha uhakiki wa vipimo cha Misugusugu. Kituo hicho ni moja ya vituo vya kisasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambacho kina uwezo wa kupima matenki ya malori 60 kwa siku.

Alisema, kituo cha Misugusugu kimefanikiwa kuhakiki tenki 21,746 ambapo ndiyo hutumika kusafirisha shehena ya vimiminika toka bandari ya Dar es Salaam na kwenda mikoani au nchi za nje kama vile Zambia, Rwanda, Malawi, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Wakala wa Vipimo inaendela kutoa huduma za uhakiki wa kiasi cha mafuta (Jamii ya Petroli na Mafuta ya Kula) yanayoingia nchini kupitia bandari za Dar es salaam, Tanga na Mtwara,” alisema.

Kihulla aliongeza kuwa, WMA imefanikiwa kuhakiki jumla ya lita 30,645,930,571 za mafuta kwa meli 546 zilizowasili nchini.

Uhakiki huo ulifanikiwa kufuatia maboresho yaliyojumuisha kusimika mita ya kisasa katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na kuchangia kuongezeka kwa ujazo wa mafuta yaliyohakikiwa kufikia jumla ya lita 30,645,930,571 ambapo kati yake, lita 13,888,897,421 kwa ajili ya matumizi ya ndani na lita 16,757,033,150 zilisafirishwa nje ya nchi.

Alisema, Wakala imehakiki kiasi cha gesi iliyoingia nchini kwa njia ya meli ambapo jumla ya tani za ujazo 958,593.17 za gesi zilishushwa na meli 210 zilizowasili nchini.

“Katika kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Wakala inafanya ukaguzi na uhakiki wa vipimo kwenye mitungi ya gesi ili kuhakikisha kuwa wanunuzi wa gesi wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha wanayolipa kwa ajili ya huduma hiyo,” alisema Kihulla.

Vile vile alisema, Wakala imepatiwa jumla ya magari 21 ili kutekeleza kwa ufasaha kazi za uhakiki na ukaguzi wa vipimo katika maeneo mbalimbali nchi nzima, magari hayo pia yamewezesha utunzaji mzuri wa vifaa vya kitaalam.

Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, WMA imefanikiwa kufungua vituo maalum 10 katika Mikoa ya Dsm, Tanga, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya, Kagera, Kigoma na Mara kwa ajili ya kukagua bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya nchi na zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Aidha, jumla ya bidhaa 70,660 zilizoingia nchini zilikaguliwa, ambapo WMA inatarajia kuanza uhakiki wa Taxi meter na tayari mitambo 12 imeshanunuliwa; miwili ya kusimika ambapo mtambo mmoja unaendelea kusimikwa katika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu na mtambo mwingine utasimikwa katika ofisi ya Makao Makuu Dodoma.

“Mitambo mingine 10 (portable taximeter) itagawiwa kwenye mikoa kwa ajili ya kuhakiki vipima mwendo kwenye vyombo vya usafiri,” alisema.

Kihulla alisema, Wakala imejipanga kuendelea kufungua ofisi sehemu mbalimbali zinazooneka kuwa na ukuaji wa shughuli za ukuaji wa kiuchumi na kijamii ili kuendelea kuwalinda watoa huduma na wapokea huduma kupitia matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa.

Sambamba na hilo alisema, WMA itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na matumizi sahihi ya vipimo kwa kutumia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na kushiriki kwenye maonesho na makongamano mbalimbali ili wananchi wazidi kuifahamu Wakala wa Vipimo, majukumu yake, na umuhimu wa kutumia vipimo sahihi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here