Wekeni nguvu katika kutoa elimu ya fedha – Dkt. Mpango

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mabenki kubuni mipango mbalimbali ya utoaji wa elimu kwa umma na kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza uelewa juu ya masuala ya kifedha pamoja na umuhimu wa kutumia huduma za benki.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Tawi la Benki ya CRDB – Buhigwe mkoani Kigoma.

Alisema, elimu na uelewa kuhusu masuala ya fedha umeonekana kuwa mdogo miongoni mwa wananchi kitu kinachopelekea baadhi yao kushindwa kufahamu kuhusu bidhaa na huduma za kifedha zilizopo na ushirikiano uliopo kati ya watoa huduma za fedha na umma.

Ametoa rai ya kuendelea kuwapa wateja na wananchi wote kwa ujumla, elimu juu ya umuhimu wa kuweka akiba, kukopa na kurejesha na kutumia fedha walizokopa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, alisema ni vema Wananchi waelimishwe umuhimu wa kuwa na akaunti benki ili fedha zao ziweze kuwa salama na wakifanya malipo kupitia benki wanajijengea historia nzuri ya kukopesheka.

Vilevile, Makamu wa Rais ameipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake katika kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema, kampeni shirikishi zinazotekelezwa na Benki hiyo zinatoa hamasa kwa wananchi na taasisi nyingine, ikiwemo sekta binafsi kuunga mkono jitihada za Serikali katika uhifadhi wa mazingira.

Amewasisitiza kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana na Wana-Buhigwe katika kufadhili miradi ya kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema, Wilaya hiyo yenye hazina kubwa ya uoto wa asili, inakabiliwa na tishio kubwa la athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makamu wa Rais amesema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya jitihada za Serikali kusimamia mageuzi makubwa na maboresho ya mazingira ya biashara, ili kuhakikisha sekta ya benki inakua na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Alisema, Serikali imeendelea kuwezesha ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya fedha, hatua iliyozaa mafanikio makubwa, kama vile huduma za kibenki za kidijitali, huduma za fedha kupitia simu, huduma za kibenki mtandaoni, na pia huduma za uwekezaji kama vile Hatifungani ya Kijani, Hatifungani ya Miundombinu ya Samia na Hatifungani ya Sukuk.

Halikadhalika, Makamu wa Rais ameongeza kwamba, kupitia sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha na Mfumo wa Ujumuishi wa Kifedha, Serikali imejipanga kupunguza idadi ya Watanzania wasiofikiwa na huduma rasmi za kifedha, hususan vijijini.

Aidha, Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA, ikiwemo kuimarisha mkongo wa Taifa wa mawasiliano na kupunguza gharama za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha za kidijitali kwa urahisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here