WCF yatimiza miaka 10 kwa kutaja mafanikio matano

0

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wameweka wazi mafanikio ambayo yamepatikana ndani ya miaka 10 tangu ulipoanzishwa na miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Kaduma, alitaja mafanikio hayo wakati wa mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Mei 15, 2025 jijini Dar es Salaam ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina (TR).

Kaduma alisema, WCF imefanikiwa kuwalipa wafanyakazi na wategemezi wao wapatao 19,650 waliopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi “hili ni hitaji la msingi la uanzishwaji wa Mfuko na linaonyesha utendaji wa moja kwa moja wenye tija kwa jamii ya wafakazi.”

Aidha, Dkt. Kaduma alisema mafanikio mengine ambayo wameyapata ni kuongeza mafao saba makuu ambayo ni pamoja na Fao la matibabu (bila kikomo), Fao la ulemavu wa muda mfupi, Fao la ulemavu wa kudumu, Fao Pensheni kwa wategemezi, Fao la wasaidizi wa mgonjwa, Fao la utengamano na Fao la msaada wa mazishi.

Mafanikio mengine ambayo WCF wameyapata ni uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, mfuko huo hivisasa umetekeleza mapinduzi wa kidigitali kwa zaidi ya 90% ambapo huduma zote zinapatikaba kwa njia ya mtandao “Mifumo hii imepunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuboresha ufanisi wa utendaji kazi.

Mbali na mafanikio hayo, Dkt. Mduma alisema Juni, mwaka 2024 WCF ilipata cheti cha, ithibati cha ISO (ISO Certification) kwa utoaji wa huduna bora kwa viwango vya Kimataifa, jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa mfuko huo kuwapa matumaini wadau wao.

Pia, mwaka 2023 mfuko huo ulipata tuzo ya ISSA (International Social Security Association) kwa matumizi bora ya TEHAMA na mwaka huu 2025, WCF ilishika nafasi ya pili katika tuzo za eGA na nafasi ya tatu kwenye Tuzo za TEHAMA 2025 kwa taasisi za umma zilizofanikiwa kuondoa urasimu kupitia TEHAMA.

“Vile vile mfuko umeendelea na kampeni mbalimbali za elimu na uhamasishaji kwa waajiri na wafanyakazi juu ya haki zao, taratibu za fidia na usalama mahali pa kazi. Elimu hii imesaidia kupunguza ajali na magonjwa kazini, pamoja na kuongeza usajili wa waajiri,” alisema Dkt. Kaduma.

Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo, Dkt. Kaduma alisema, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo wanaendelea kuzifanyia kazi ikiwemo waajiri kutosajili na kuwasilisha michango kwa wakati.

“Baadhi ya waajiri bado hawajatekeleza matakwa ya sheria ya kuwasajili wafanyakazi na kuwasilisha michango kila mwezi. Hili linawanyima haki wafanyakazi wanapopatwa na majanga kazini,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa WCF alisema, licha ya changamoto hizo mfuko huo umeendelea kujidhihirisha kuwa ni chombo muhimu cha ulibzia wa kijamii kwa wafanyakazi nchini.

Aidha, WCF umekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika, na Shirika la Kazi Duniani (ILO) wamezishauri nchi mbalimbali kujifunza jinsi unavyoendeshwa na alizitaja nchi ambazo zimefika nchini ni pamoja na Kenya, Zambia, Malawi na Ethiopia.

“Eswatini tuna miadi nao, wanataka kuja kujifunza, Afrika Kusini tulibadilishana nao uzoefu maana wao wana miaka 20 katika kuwalipa fidia wafanyakazi, walitushauri kutumia Akili mnemba (Artificial Intelligence), nasisi wamejifunza kumtambua mwajiriwa na mwajiri, wao kwasasa wanamtumua mwajiri,” alisema.

Dkt. Kaduma kupitia mkutano huo alisisitiza kuwa, wataendelea kuboresha huduma, kushirikiana na wadau wote na kuhakikisha wanasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi ili kila mfanyakazi anapopatwa na madhira anapata haki yake kwa wakati.

“Natoa wito kwa waajiri wote kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kwa wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wakijua kuwa mfuko wao uko imara na thabiti kuwahudumia,” alisisitiza Dkt. Mduma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here