Waziri Mkuu ataka mwendokasi BRT -2 kuanza mwezi huu

0

Na OR- TAMISEMI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Waendeshaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha maeneo yaliyobaki ili mradi uanze kutoa huduma mara moja ndani ya mwezi huu.

Maelekezo hayo ameyatoa Agosti 13, 2025 wakati akikagua mabasi mapya ya awamu ya pili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT-2) pamoja na miundombinu ikiwemo kituo kikuu cha mabasi hayo cha Mbagala Rangi tatu na kituo cha Gerezani jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mabasi yaliyo katika bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa kituo maalum cha kujazia gesi kwa ajili ya mabasi hayo, kinachojengwa katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu Mradi wa BRT-2 amesisitiza kukamilisha kazi zilizosalia kwa haraka ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kufurahia huduma hiyo muhimu

“Nawataka mkamilishe kazi hii mara moja ndani ya mwezi huu ili wananchi waweze kupata huduma hii ya usafiri wa kisasa ambao Serikali imeamua kuwaletea wananchi” ameelekeza Majaliwa.

Aidha, ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kunatarajia kuongeza ufanisi wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kutoa huduma ya kisasa, salama na ya haraka kwa wananchi

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi pamoja na watendaji wengine wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here