Na Abel Kiharo
“Mzee anapofariki, maktaba yenye maarifa ya kutosha inakuwa imeanguka chini.” Huo ni moja ya usemi wa Kiafrika unaoonyesha umuhimu wa wazee ndani ya jamii zetu.
Mzee ni maktaba inayoishi, mzee ni dhahabu iliyopo eneo la wazi na mzee ni kisima cha maarifa ambacho ukienda kuchota maji huko utakutana na hekima ya ajabu.
Wale watu wenye hekima waliwahi kusema kuwa “Ukimuona nyani aliyezeheka, ujue amekwepa mishale mingi.” Ukweli ni kwamba; ukimuona mwanadamu aliyezeeka, ujue amekutana na changamoto nyingi katika maisha yake mpaka kufika hapo alipo.
Ni neema kuufikia uzee na ni baraka zaidi kuufikia uzee mwema. Hatua ya kuufikia uzee ni hatua ya kuheshimika. Haijalishi aliyezeeka ni tajiri au maskini, ukweli ni kwamba; anajua mambo mengi zaidi kuliko vijana.
Mzee anatosha kuwa sababu ya vijana wengi kupata hekima na kuishi kipindi cha ujana wao wote kwa mafanikio makubwa. Wazee ni tunu kwa vijana.
Faida kubwa anayoweza kuipata mtu kwa mzee ni kujifunza kutokana na yale aliyoyapitia mzee huyo, enzi zile za ujana wake. Tukiyafahamu makosa ambayo wenzetu waliwahi kuyafanya enzi za ujana wao, inakuwa rahisi kwetu kuyaepuka katika kipindi hiki cha ujana wetu.
Kurudia makosa yaleyale ambayo yaliwahi kufanywa na wengine huko nyuma, ni kuudhihirisha uzembe tulionao wa kutafuta maarifa kutoka kwao.
Sababu kubwa inayosababisha mmomonyoko wa maadili kwa vijana wengi ndani ya jamii zetu, ni kushindwa kuwa karibu zaidi na wazee. Kama vijana wangenyenyekea kwa wazee na wakakubali kujifunza kutoka kwao, tungekuwa na jamii zenye vijana wenye hekima sana.
Kiburi walichonacho vijana wengi, ndiyo sababu kubwa inayoendelea kuwazuia kupata mafanikio makubwa maishani mwao.
Zamani ndoa nyingi zilidumu ikilinganishwa na sasa, hii ni kwasababu wale waliooana yalikuwa ni matunda ya hekima waliyoivuna kwa wazee wao. Lakini, ulimwengu huu tulio nao sasa, vijana wengi wanaamini tayari wanajua, matokeo yake ndiyo hayo ndoa nyingi zimekuwa zikifungwa kwa shangwe kubwa leo, halafu kesho asubuhi zinavunjika!
Ni muhimu vijana turudi kwenye misingi ya Waafrika. Bado tunayo mambo mengi ya kujifunza kwa wakubwa zetu waliotutangulia. La sivyo, tunajiandaa kukosa majibu sahihi ya maswali magumu tutakayokutana nayo kutoka kwa watoto wetu.
Kujitenga na wakubwa, itatufanya tuwe katika hatari kubwa ya kufanya makosa ambayo tungeweza kuyaepuka kiurahisi.
Haina maana kwamba wazee ni malaika. Wala simaanishi kila neno litokalo kinywani mwa mzee ni lenye hekima. Lakini, sehemu kubwa ya kile kitokacho kwao ni chenye hekima, hasa pale wanapokuwa wameombwa msaada wa kimawazo.
Mzee anaielewa picha kamili ya dunia hii, anaelewa kwa sehemu kubwa kuhusu mwenendo wa maisha ya mwanadamu.
Uzee ndicho kipindi maalum cha kujipongeza au kujilaumu. Mzee aliyeutumia ujana wake vizuri, hukitumia kipindi cha uzee wake kuifurahia misingi bora aliyojiwekea enzi za ujana wake.
Kijana ukiwa karibu sana na mzee huyu, atakufundisha namna ya kuweka misingi yako imara katika maisha yako ukiwa bado kijana. Mzee wa aina hii anazielewa siri nyingi za ushindi!
Mzee aliyeutumia ujana wake vibaya, hukitumia kipindi cha uzee wake akijilaumu na kujutia makosa aliyoyafanya kipindi cha ujana wake. Kama kijana ukiwa karibu zaidi na mzee huyu, utayaelewa vizuri makosa aliyoyafanya na itakuwa ni rahisi sana kwako kuyaepuka makosa ya aina hiyo katika ujana wako.
Kipindi cha ujana ndicho kipindi cha kukutana na changamito nyingi sana, kama usipokuwa makini, utajikuta unaangushwa na changamoto hizo na hatima yake itakuwa ni maisha yako kupoteza mwelekeo kabisa.
Lakini, ukiwa makini utakivuka kipindi cha ujana wako ukiwa na ushindi mkubwa na hatima yake utaondoka duniani ukiwa kama shujaa. Njia moja wapo ya kuupata umakini huu ni kuwa karibu zaidi na wazee.
Kwa kawaida kijana anayo kasi kuziendea ndoto zake, lakini mzee ndiye anayeelewa vyema njia sahihi iko wapi ya kumfikisha kijana huyo kule anapotamani kufika.
Ukiwa karibu na mzee mwenye hekima, zile hatua unazozipiga kila siku kuziendea ndoto zako zitakuwa na thamani zaidi. Tofauti na hapo, unakuwa umetengeneza mazingira makubwa ya kuishia kwenye ubatili.
Mpaka sasa tunaendelea kuwaona wazee kama watu wa kawaida mno! Lakini, uhalisia ni kwamba, hawa watu wamebeba vito vingi vya thamani ndani yao kwa ajili yetu. Tutakapojua kuwatumia vyema, hatutaweza kusalia kama tulivyo siku zote.
Kama wewe ni mfanyabiashara, watafute wale wazee waliowahi kufanya biashara enzi zao (au bado wanafanya biashara) hakikisha unavuna hekima za kibiashara kutoka kwao.
Kama wewe ni mwalimu, daktari, mwanasheria, mkulima n.k. watafute wale wazee ambao tayari washawahi ifanya kazi hiyo, waulize yale maswali ambayo haujui majibu yake juu ya eneo hilo, kiasi ambacho unaamini majibu ya maswali hayo yatakuongezea ufanisi katika eneo lako. Hii njia inaweza kukuletea matokeo makubwa sana!
Ile changamoto unayoipitia sasa, wapo wengine ambao waliwahi ipitia huko nyuma. Watu hawa wanazo mbinu za kutosha, ambazo zinaweza kukusaidia kuishinda changamoto hiyo, hakikisha unakuwa karibu yao.
*Mwandishi wa makala hii ni Mkufunzi wa Vijana na Mjasiriamali. Kwa maoni, ushauri au maswali usisite kuwasiliana naye kwa anuani zifuatazo:- Barua pepe: kiharoabel@yahoo.com. Simu: +255628733839/+255767180002. WhatsApp: +255767180002.