Na Benny Mwaipaja, Washington DC
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa wawekezaji wa Kimataifa pamoja na wazawa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini Washington D.C, Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi anayesimamia masuala ya masoko ya mitaji, maendeleo ya Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Sarvesh Suri, ambapo Dkt. Nchemba anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Alisema, Serikali inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara ili kuchochea uwekezaji na kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje ya nchi na kuiomba taasisi hiyo itoe dhamana kwa kampuni, taasisi au mashirika yanayotaka kuwekeza nchini Tanzania.
“Tuna maeneo ya uwekezaji kwenye nishati, reli ya kisasa, kilimo, utalii na miundombinu ya barabara ambayo ni fursa kwa uwekezaji” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema, Tanzania iko katika eneo la kimkakati kijiografia kwa kuwa inapakana na nchi nyingi zisizo pakana na bahari na pia inajivunia uwepo wa soko la uhakika la bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Aidha, aliiomba Taasisi hiyo ya MIGA itoe dhamana kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu ili wawekeze kwenye maeneo hayo ambayo yatawapatia faida na kukuza ajira.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba, alisema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za kurekebisha sheria ya kulinda uwekezaji ambayo ikikamilika itachochea zaidi uwekezaji.
“Tumepeleka rasimu ya sheria hiyo ya uwekezaji bungeni na hivi sasa tunakusanya maoni ya wadau na baadae itawasilishwa tena bungeni na tunatarajia sheria hiyo ikipitishwa itaondoa urasimu wa mchakato wa uibuaji miradi ya PPP na pia kulinda uwekezaji,” alisema Bw. Tutuba.
Kwa upande wake Mkurugenzi anayesimamia masuala masoko ya mitaji, maendeleo ya Nishati na Mabadiliko ya Tabia wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Sarvesh Suri, aliipongeza Tanzania kwa hatua zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji ambayo yameanza kuwavutia wawekezaji wengi wanaotaka kuwekeza nchini kupitia taasisi yake.
Alisema, kongamano la uwekezaji Barani Afrika lililofanyika Dar es Salaam Septemba 14-15, 2022 na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika kujadili fursa na changamoto za uwekezaji barani humo, umewavutia wawekezaji wengi.
Suri alisema, wadau hao wameonyesha nia ya kuwekeza mitaji yao na kuiwezesha Tanzania kujulikana, hatua itakayochangia kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na maisha ya watanzania.
Mkurugenzi huyo alisema, Sekta Binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani na kwamba, mazingira mazuri ya uwekezaji yanayofanywa na Tanzania kupitia mabadiliko ya sheria mbalimbali zilizokuwa zinakwaza uwekezaji wa mitaji na teknolojia nchini, yatakuza uwekezaji huo.