WATANZANIA wameahidiwa mambo makubwa zaidi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ikiwemo kupata huduma za uhakika kwenye ofisi za Mfuko huo sambamba na kwenye vituo vya utoaji wa huduma vilivyopo sehemu mbalimbali nchini.
Hivi sasa, NHIF ina jumla ya vituo 9,467 vilivyosajiliwa ili kutoa huduma kwa wanachama wake, ambapo kati ya vituo hivyo 6,852 sawa na asilimia 72 ni vya Serikali huku vituo binafsi vikiwa ni 1,766 sawa na asilimia 19, na vituo vya madhehebu ya dini ni 849, sawa na asilimia tisa.
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga alisema hayo kwenye kikao kazi kilichowahusisha wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.
Konga alisema, kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mfuko huo umepata mafanikio mengi, hivyo mipango waliyonayo ni kuboresha huduma zao na kupata mafanikio makubwa zaidi.
“Hadi kufikia Machi mwakani, mipango yetu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya wanachama sambamba na kuimarisha huduma zetu. Pia, tutahakikisha huduma zinapatikana bila vikwazo na mfuko unakuwa endelevu na unakuwa na ustahimilivu”, alisema Konga.
Aliendelea kusema, mipango mingine waliyonayo ni kuwa Taasisi yenye mchango mkubwa kwa Taifa ikiwemo kukuza uchumi, kwani iwapo wananchi watakuwa na afya njema, watafanya shughuli zao za kujipatia kipato na kuinufaisha nchi.
“Tunataka mwananchi asiuze bodaboda yake au shamba kwa ajili ya kulipia matibabu,” alisisitiza Konga, huku akihimiza wananchi wajiunge na Mfuko huo na wawe tayari kwa Bima ya Afya ya Pamoja.
Alisema, licha ya changamoto iliyopo ya mwamko mdogo wa wananchi kujiunga na bima, lakini wana matumaini makubwa ya kupata wanachama wengi zaidi kutokana na hamasa na elimu wanayoitoa kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya Kijamii.
“Uhalisia unaonesha kuwa asilimia 85 ya Wananchi hawana Bima ya Afya na hivyo kukosa uhakika wa huduma bora za afya kipindi wanahitaji,” alisema na kuongeza kuwa, chimbuko la kuandaliwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kutimiza wajibu wa Serikali wa Kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.
Konga alisema, wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kama runinga na Radio ambapo matangazo 1,268 ya elimu ya NHIF yalirushwa na makala 52 ziliandikwa magazetini.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, pia wametoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ambapo ujumbe wa elimu 834 umewekwa kwenye mitandao ya mfuko na ya wadau wengine.
Aidha, wamekuwa wakishiriki kwenye maonesho 11 na kutoa elimu kama Sabasaba na Nanenane ambapo watu 17,153 walipewa elimu na watu 4,131 walijiunga na mfuko huo.
“Mfuko ulifanya mikutano 47 na wadau mbalimbali wa mfuko ikiwa ni pamoja na watoa huduma na wanachama katika mikoa mbalimbali. Jambo jingine ni kuendelea kutekeleza mikakati ya utoaji elimu kwa umma kuhusu dhana na umuhimu wa kuwa na bima ya afya,” alisema Konga.