Watanzania waongoza kwa kuchangamkia zabuni

0
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Dennis Kwame Simba

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema, watanzania wanaongoza kwa kupewa zabuni mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA  Dennis Kwame Simba amesema hayo leo Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa vyombo ya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Simba alisema, hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024, wazawa  36,989 ambayo ni sawa na asilimia 99.6 walipata zabuni, China walipata  28, Kenya  21, Afrika  Kusini 18, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) 10.

Alisema, katika kuwaongezea nguvu wazabuni wa ndani, sheria mpya ya ununuzi wa umma imeweka fursa ya wazabuni wa nje (partnership) na kwa ushiriki huo, kampuni ya ndani ndiyo itakuwa kampuni kiongozi na feha zitalipwa kwa kampuni ya  ndani “zabuni zenye thamani isiyozidi Shilingi Bilioni 50 zimetengwa kwa ajili ya wazabuni wa ndani ya nchi.”

Mbali na kuwawezesha wazabuni hao, Mkurugenzi huyo alisema, sheria ya manunuzi ya umma Sura 410, inazitaka Taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Alisema, tangu mfumo wa NeST ulipoanza kutumika Julai 1, 2023, hadi Oktoba 8, 2024, jumla ya vikundi 210 vilifanikiwa kupata tuzo za zabuni zenye thamani zaidi ya Bilioni 9, katika mwaka wa fedha uliopita, kuanzia Julai 1 hadi Juni 30, 2024, vikundi 85 vya vijana vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.

Aidha, katika makundi mengine  tangu Julai 1, 2023 hadi Juni 30, 2024, vikundi 84 vya wanawake vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 4 na vikundi viwili vya wazee vilipata zabuni zenye thamani ya Shilingi Milioni 78.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alisema, hadi kufika Oktoba 31, 2024 jumla ya taasisi nunuzi 21,851 zimesajiliwa na zinatumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) “ bajeti ya ununuzi ya zaidi ya Shilingi Trilioni 38.6 imewekwa kwenye Mfumo wa NeST, kama fursa ya wazi kwa ajili ya wazabuni.”

Alisema, wazabuni zaidi ya 28,590 wamejisajili kwenye Mfumo wa NeST huku mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 10.2 imetolewa kwa wazabuni kupitia  Mfumo wa NeST.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here